Na Mwandishi Wetu
Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Urais, Wabunge na Madiwani zinaendelea kutikisa katika kila kona ya nchi kwa wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa wakinadi ilani zao cha uchaguzi.
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuvutia maelfu ya wananchi ambao wamekuwa wakimiminika katika mikutano yake.
Shahuku hiyo ya wananchi ni matokeo ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) kwa mafanikio makubwa hali ambayo imeendelea kujenga matumaini kwa Watanzania kukiamini zaidi CCM kupitia mgombea wake wa Urais.
Hata hivyo, miongoni mwa matukio ya kipekee kwenye kampeni hizo ni namna ambavyo viongozi wakuu wastaafu ndani ya Chama na serikali walipopanda katika majukwaa ya kampeni hizo kumnadi Dk. Samia kwa kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana.
Kipyenga cha kampeni hizo, kilipulizwa Agosti 28 mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers ambapo, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, alianza kufungua pazia kwa kuwaleza wananchi.
Alisema Dk. Samia alipokea nchi katika kipindi kigumu baada ya kufariki dunia aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli.
Alieleza kuwa hofu ilitanda kama ataweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo baadhi kwa bahati mbaya haikuwa katika bajeti ya serikali.
“Miaka mitano baadaye, ametuthibitishia pasi na shaka kwamba ameyaweza mamlaka ya Urais na Amiri Jeshi Mkuu. Nchi imeendelea kuwa yenye amani, umoja, mshikamano na maendeleo yanaonekana. Ikumbukwe kwamba marais wote tuliopita tangu vyama vingi tulikuwa na muda wa kujiandaa.
Aliongeza: “Tulipata muda wa kuunda timu, watu na sera. Lakini yeye (Dk. Samia) aliipokea nchi katika hali tofauti.”
Kikwete alisema baada ya miaka minne Dk. Samia amedhihirisha ni kiongozi mwenye maono ya mbali akiwa na ubunifu wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Alisema moja ya ubunifu huo ni falsafa ya 4R ambayo imekuwa chachu ya kuimarisha maendeleo, kustawisha amani, umoja, utulivu na kuimarisha muungano.
Pia, alisema kiongozi huyo aliweza kulitoa taifa katika kipindi kigumu wakati wa mripuko wa ugonjwa wa UVIKO – 19.
Alisisitiza kuwa ubinifu aliokuja nao wakati wa ugonjwa huo ni kutumia fedha zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kugusa maisha ya Watanzania.
“Nchi za Afrika na baadhi ya zile zilizoendelea walitumia fedha hizo kutoa ruzuku kwa wafanyabiashara lakini siyo kunufaisha wananchi,” alisema.
Alieleza kuwa fedha ambazo zilizotumika nchini ziliwagusa Watanzania kupitia ujenzi wa shule na ununuzi vifaa vya hospitali.
“Ametekeleza kwa vitendo dhamira ya kumtua ndoo mwanamke kichwani. Wanawake hawasumbuki tena. Ameleta mabadiliko ya ukusanyaji kodi. Mapato yameongezeka na sasa wafanyabiashara hawafikirii tena kuondoka nchini,” alisisitiza.
Alisema Dk. Samia amesimamia vyema mahusiano na viongozi wa dini kwani amekuwa akithamini haki za binadamu ikiwemo kuanzisha tume ya haki jinai.
Rais huyo mstaafu alisema kuthamini haki za binadamu ndiyo chanzo cha kauli mbiu ya CCM ambayo ni “Kazi na Utu, Tunasonga mbele.”
STEPHEN WASIRA
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wassira naye aliumia jukwaa hilo kuwaeleza wananchi kwamba Rais Dk. Samia anastahili kupewa ridhaa ya kuongoza taifa kwani amefanikiwa kulivusha salama taifa katika kipindi kigumu aliposhika hatamu ya uongozi wa nchi.
Wassira alisema kiongozi huyo alipokea madaraka nchi ikiwa inakabiliwa na majaga matatu.
Aliyataja majanga hayo ni Uviko 19, kuporomoka uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia nne na janga la nchi kuondokewa na Rais Hayati Dk. Magufuli akiwa madarakani.
“Pamoja na majanga hayo Rais Dk. Samia aliwezea kuivusha nchi salama, kuchangia kuimarika umoja wa Watanzania na nchi kuendelea kuwa yenye amani.
“Alitumia muda wake kukutana na makundi mbalimbali ikiwamo vyama vya siasa na jukwaa la wahariri na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizoelezwa na makundi hayo,” alibainisha.
Wassira alisema Dk. Samia alitekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Alitaja mradi mwingine ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake unandelea.
Vilevile, alisema Dk. Samia amejenga shule, vituo vya kutolea huduma za afya na kutolea mfano kwa Dar es Salaam pekee shule 224 za sekondari zimejengwa ndani ya miaka minne.
JOHN MALECELA
Mwanasiasa kongwe ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee John Malecela, aliungana na viongozi wenzake kueleza kwanini Mkoa wa Dodoma unapaswa kumpa kura za kishindo Rais Dk. Samia.
Alisema mkoa huo umekuwa na historia tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi kuongoza kwa idadi ya kura nyingi kwa wagombea Urais kupitia CCM.
“Napenda kuchukua nafasi kumshuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amechaguliwa kugombea Urais kupitia CCM. Niwaeleze huko nyuma ukienda kuangalia kwenye rekodi tangu Tanzania tuanze kuwa huru kuchagua viongozi wetu wa nchi ambaye ni Rais, kuna mikoa miwili ambayo imekuwa na rekodi nzuri tangu tuanze uchaguzi.
“Mikoa hiyo ni Iringa na Dodoma, sasa mimi nina jambo moja la kuwaomba Wanadodoma wenzangu, rekodi za huko nyuma zinaonyesha kwamba kila mara tumekuwa tukiwapa Marais wetu wagombea kura nyingi kuliko mikoa mingine, sasa niwaombe safari hii ndugu zangu wote Mkoa wa Dodoma, nina uhakika kwamba wananchi wote tutampa kura zetu Dk. Samia,” alisema.
DK. MPANGO
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango alifunguka namna ambavyo baadhi ya wananchi katika mataifa mbalimbali duniani wanavyotamani kuwa na kiongozi aina ya Dk. Samia.
“Kule unaponituma wenzetu wanatamani huyu awe Rais wao, nawasihi sana Oktoba 29 mwaka huu mkampigie kura Mama Samia mitano tena,” alieleza huku wananchi wakiitikia mitano tena.
MZEE MANGULA
Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara, Mzee Philip Mangula alisema Watanzania anapaswa kumpigia kura Rais Dk. Samia ili akamalize mazuri ambayo ameendelea kuyafanya kwa maslahi ya Watanzania.
“Ukiwa unaingia kwenye gari unatakiwa kuangalia anayekuendesha kwani wengine wanaweza kuwa ‘malena’ lakini ni tofauti kwa Rais Samia kwani ana leseni ya kimataifa ambayo inamfanya awe na uzoefu katika kuendesha.
DK. BASHIRU
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk. Bashiru Ali alisema nguvu ya CCM inatokana na umoja ndani ya Chama huku akimpongeza Rais Dk. Samia kuliunganisha taifa.
“Nakushukuru Mwenyekiti kwa kuchukua kazi hii na umeisimamia kuunganisha vizuri nchi yetu inaendelea kufanya vizuri katika maeneo mengi, tupo kuwanadi wagombea kutokana wa ilani na utendaji wetu bora. Tunaomba sana muendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi na Dk. Samia,” alisema.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adamu Kimbisa alisema wamekuja na bidhaa adimu ambayo ni Samia Suluhu Hassan, hivyo amewaomba wananchi kumpigia kura ifikapo Oktoba mwaka huu.
Akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Dk. Samia alisisitiza Tanzania itakuwa nchi yenye neema itakayotekeleza miradi ya maendeleo pasipo kutegemea mikopo mikubwa huku wananchi wakipata huduma bora za afya, elimu, umeme wa uhakika.
Alisema safari hiyo ya mafanikio itafikiwa katika miaka mitano ijayo hivyo amewaomba Watanzania kukipigia kura CCM kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu ili kufanikisha neema hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Mvomero eneo la Dakawa mkoani Morogoro, Dk. Samia alisema CCM ina historia ya utekelezaji ilani kwa mafanikio makubwa.
“Niwaombe tusimame pamoja kuiunga mkono CCM tuendelee na kasi kujenga Tanzania tunayoitaka. Tukifika mwaka 2050 (kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya taifa 2050) tuwe tumeifika Tanzania yenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu. Hakuna Mtanzania atakayelia kukosa huduma za afya, elimu wala kukosa umeme.
Alisisitiza: “Tutakuwa na Tanzania ambayo uchumi wake utasimama kujitegemea, hatutaishi wala kufanya shughuli za maendeleo kwa mikopo mikubwa. Na hiyo safari tunaanza miaka mitano inayokuja.”
AHADI SIKU 100
Wakati akizindua kampeni, Dk. alitaja vipaumbele muhimu atakavyovitekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa.
Alisisitiza kuwa serikali atakayoiunda itajikita kuleta mabadiliko yenye kugusa maslahi ya wananchi moja kwa moja katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Miongoni mwa mambo ambayo ameahidi kuyatekeleza ndani ya siku 100 ni kutoa ajira 12,000 kwa walimu na wataalamu wa afya, serikali kutoa matibabu bure kwa wajawazito, wazee na Watoto kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote.
Dk. Samia alisema serikali yake itapiga marufuku hospitali kuzuia miili ya ndugu zao kwa madai ya kutolipa gharama za matibabu.
“Kupitia Bima ya Afya kwa Wote, tutazindua mfumo wa mfumo wa taifa kwa wamu ya majaribio kuanzia wazee, wototo, wajawazito ambapo gharama za matibabu zitabebwa kupitia mfuko wa bima ya afya.
“Pia, serikali itagharamia kwa asilimia 100 wananchi wasiokuwa na uwezo kupata vipimo vya figo, moyo, sukari, mishipa ya fahamu na mifupa. Tutatoa ajira 5000 katika sekta ya afya ndani ya siku 100 wakiwemo wauguzi na wakunga.
Alisisitiza: “Tutapia marufuku hospitali kuzuia miili ya marehemu kuchukuliwa kwa sababu ya kudaiwa gharama za matibabu. Tutakuja na mfumo mwingine kuhakikisha jamaa wa marehemu wanalipa gharama lakini siyo kuzuia miili.”
Dk. Samia alisema ndani ya siku 100 serikali yake itaweka mkakati wa elimu kisayansi ambao kila mtoto wa darasa la tatu atakuwa na uwezo wa kusoma, kuandika bila shida, sambamba na kuajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi.
“Tutazindua mpango wa Pamoja utakaohusisha waajiri, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele. kuwafanya wanafunzi wa VETA kuchukuliwa viwandani kufanyakazi zao za mazoezi.
“Tutatenga sh. bilioni 200 kuwezesha upatikanaji mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na kati, uanzishwaji kampuni changa, kurasimisha wajasiriamali wadogo wakiwemo bodaboda, mama lishe, wafanyaviashara wadogo kuingizwa katika mfumo rasmi wa serikali.
Vilevile, alisema serikali itaanzisha programu ya mitaa ya viwanda wilayani kwa lengo la kuzalisha ajira kupitia mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi madini na misitu.
Pia, alisema katika siku hizo, serikali itakayoiunda itaanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji kwa lengo la kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji.
Alisema gridi hiyo itahusisha vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni Ziwa Viktoria, Tanganyika, Nyasa na mito mikubwa.
Ahadi nyingine aliyoitoa ni kuendeleza jitihada nishati safi kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuweka mifumo rafiki ya uwajibikaji kwa
mawaziri na wakuu wa mikoa kutakiwa kutoa taarifa na kujibu maswali kwa wananchi kwa njia ya simu.
“Kuendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi ikiwemo kuunda tume maalum kundaa mazingira ya mchakato wa katiba mpya.
Dk. Samia alizitaja sababu kuu mbili zilizomfanya kugombea nafasi hiyo ambazo ni tumefanya vyema na kufanikiwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Chama kuamini uwezo wake katika kulitumikia Taifa.