Mwamvua Mwinyi, Pwani
Pwani, Septemba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, amepokea magari manne ambapo ameishukuru Serikali na kusema yataongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha usimamizi wa shughuli za kiusalama katika ngazi ya mkoa na wilaya.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya magari hayo mkoani Pwani, Morcase alisema magari hayo yatatumika katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa pamoja na Wilaya za Kisarawe, Bagamoyo, Chalinze na Mlandizi.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, kwa msaada wa magari mapya yaliyotolewa kwa Jeshi la Polisi mkoani Pwani”
“Magari haya yatasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku, hasa katika kuwafikia wananchi kwa haraka na kwa wakati wanapohitaji msaada wa kiusalama,” alieleza Morcase.
Aidha, Kamanda huyo alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lina wajibu wa kuhakikisha magari hayo yanatunzwa, kuyalinda na kuyatumia kwa matumizi sahihi, kwa mujibu wa maelekezo ya viongozi wa juu wa Jeshi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kisarawe, Mrakibu wa Polisi Imelda Mwakilembe alitoa shukrani kwa IGP Camillus Wambura kwa juhudi zake katika kuhakikisha vitendea kazi vinafika kila sehemu ya nchi.
Aliahidi kuzingatia maagizo yote yaliyotolewa ili kuongeza ufanisi wa kazi katika maeneo yao ya uwajibikaji.
Mgawanyo wa magari hayo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuboresha vitendea kazi kwa maafisa wa polisi nchini, kwa lengo la kuongeza kasi ya utoaji wa huduma bora za ulinzi na usalama kwa wananchi.