NA JOHN BUKUKU- IRINGA
MJUMBE wa Kamati ya Siasa wa Mkoa wa Iringa, Dk. Tumaini Msowoya amesema kuwa wananchi wa mkoa huo wamejipanga kumpa kura za ndiyo kwa zaidi ya asilimia 90, Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Dk. Msowoya ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika mkoani Iringa, ambapo Dk. Samia aliendelea kuomba kura za wananchi.
“Sisi Iringa tutampa kura za kutosha. Nataka niwambie, tutakuwa wa kwanza kwa ushindi mkubwa. Mkoa wa Iringa ni ngome ya CCM, na tutaiendeleza ngome hii. Uchaguzi uliopita mwaka 2020 tuliongoza, safari hii tutakuwa wa kwanza tena,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wa Iringa wamekuwa mstari wa mbele kushiriki uchaguzi, kwani kuna kata ambazo waliojiandikisha kupiga kura walipiga wote isipokuwa wagonjwa na waliopoteza maisha.
Akizungumzia uongozi wa Dk. Samia, Msowoya alisema wananchi wa Iringa wanamkubali si kwa sababu ya jinsia yake, bali kwa uwezo na uongozi thabiti aliouonyesha.
“Kwangu mimi binafsi, Dk. Samia ni mfano wa kuigwa. Siiti mama kwa sababu ya jinsia yake, namuita Rais kwa sababu ya uwezo wake wa kiuongozi,” alisema.
Aidha, alisema uamuzi wa CCM kumteua Dk. Samia pamoja na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, umepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa Iringa kutokana na mambo makubwa yaliyotekelezwa katika kipindi cha uongozi wake.
Akizungumzia maendeleo yaliyofanyika mkoani humo, alisema uwanja wa ndege wa Mkoa wa Iringa umeboreshwa na sasa ndege kubwa zinaweza kutua, jambo lililorahisisha usafiri wa wananchi na wafanyabiashara. Pia barabara ya kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inajengwa kwa kiwango cha lami, hivyo kurahisisha utalii na kufungua fursa za kiuchumi. Vilevile huduma za afya zimeimarishwa kwa kujengwa kwa zahanati na vituo vya afya vya kisasa karibu na wananchi.
“Wananchi wa Iringa wamempokea Dk. Samia kwa bashasha. Ziara yake imeleta matumaini mapya kwa sababu kila mmoja anajua kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi chake,” alisema.
Dk. Msowoya pia aliwahimiza vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.
“Vijana wa Iringa tusidanganyike. Siku ikifika tuamke mapema, tuwahamasishe wazee wetu na wanawake wote twende kupiga kura. Tunataka kujitokeza kwa zaidi ya asilimia 90 kulinda amani yetu na kumpa ushindi wa kishindo Dk. Samia,” alisema.
Aidha, aliwakumbusha Watanzania kuepuka kushiriki vitendo vya kuhatarisha amani, akisema CCM imeijenga na kuilinda amani kwa muda mrefu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda.
“Mama Samia, hata kama usingefanya kampeni, bado tungekupa kura. Hata helikopta zikizunguka bila wewe kuwepo, kura zetu tayari ni zako, kwa sababu tunakuamini,” alihitimisha.