Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amefunga mafunzo kwa askari 116 wa Jeshi la Akiba (Mgambo) katika hafla iliyofanyika Kata ya Mwembe wilayani humo, ambapo askari hao wamesisitizwa kuishi kwa mujibu wa kiapo walichoapa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Mgeni aliwakumbusha askari hao umuhimu wa kuzingatia maadili, akibainisha kuwa mgambo ni walinzi wa kwanza wa amani katika maeneo yao na hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii, pamoja na kupiga vita rushwa kwa vitendo.
“Serikali haitovumilia askari yeyote wa Jeshi la Akiba atakayekiuka kiapo chake. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuvuliwa cheo chake cha kijeshi,” alionya Mkuu wa Wilaya.
Pia aliwasisitiza kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki kupiga kura kwa amani na utulivu na kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 29.
Kwa upande wake, Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Same, Afisa Mteule Daraja la Pili Emmanuel Shija, alisema kuwa askari hao wameiva vya kutosha na sasa wako tayari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu kwa nadharia na vitendo.
Katika risala yao, askari hao walieleza kuwa wamejifunza masuala ya usalama wa raia na mali zao, mapambano dhidi ya rushwa, uraia na uhamiaji, utunzaji wa mazingira, usomaji wa ramani, matumizi ya silaha mbalimbali pamoja na mbinu za kivita.
Waliahidi kutumia mafunzo hayo kwa vitendo, kulinda usalama wa taifa na kuendelea kuwa chachu ya mshikamano, amani na maendeleo ya wananchi wa Same na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na mambo mengine mkuu wa wilaya huyo aliwasisitiza kuhakikisha wanaunda vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwa lengo la kuwasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za ujasiriamali.
Mafunzo hayo yalianza Aprili 16, 2025 yakiwa na jumla ya wanafunzi 135, ambapo askari 116 pekee wakiwemo wanawake 18 na wanaume 98 ndio waliofanikiwa kuhitimu, huku wengine wakishindwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu.