* Rais Dk. Samia atoa ahadi kuifungua zaidi mikioa hiyo kiuchumi.
*Kampeni zake zagusa maelfu ya wananchi.
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kudhihirisha kwa vitendo namna ambavyo kinakubalika nchini ambapo maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea kufanyika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo ni matokeo ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) kwa mafanikio ambayo Watanzania wameyashuhudia katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na utawala bora.
Mgombea Urais kupitia CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ameshafanya mikutano yake ya kampeni katika mikoa ya Morogoro, Dododoma na Songwe ambako aliwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitano kisha kutoa ahadi mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya Watanzania kama ilivyokuwa kauli mbiu ya Chama katika uchaguzi huo isemayo ‘Kazi na Utu, Tunasonga mbele.’
Akiwa mkoani Dodoma, Dk. Samia alihutubia wananchi Kibaigwa wilayani Kongwa, Chamwino, Chemba, Kondoa kisha kishindo kikuu kuhitimishwa ndani ya Jiji la Dodoma ambako mafuriko ya watu yalitawala katika viwanja vya Tambukareli huku viongozi mbalimbali wakiungana na Dk. Samia kuwaomba wananchi kura zote kwa wagombea wa CCM.
Viongozi hao ni Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee John Samweli Malecela, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Philip Mangula na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama, Balozi Dk. Bashiru Ali.
Akihutubia wananchi katika mkutano huo, Rais Dk. Samia alisema wananchi wa Dodoma wamethibitisha mkoa huo ndiyo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchapakazi huku akieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake.
“Awamu ya tano tulifanya maamuzi ya kuhamia Dodoma, awamu ya sita tumekwenda kuendeleza kuhamia Dodoma, taasisi zote za serikali zipo Dodoma, maamuzi yote makubwa sasa yanafanyika hapa.
Aliongeza: “Tumemimina sh. trilioni 9.5 kwa miradi 3,093 ndani ya Mkoa wa Dodoma, mbali na kuongeza majengo na kuipa hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa, wilaya za Dodoma zina hospitali za kisasa ambazo vipimo vyote vinapatikana huko,” alisema.
Pia, Dk. Samia alisema serikali yake imejitahidi kufungua fursa za ajira kupitia uwekezaji kwa kujenga viwanda, kutengeneza fursa kwa wafanyabiashara wadogo huku mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukiongeza kasi ya ukuaji uchumi.
Kuhusu umeme, alisema serikali inandelea na kazi ya kumalizia vitongoji ili kila mtu apate nishati hiyo kufanyakazi na kulinda usalama wao.
Kadhalika, alisema Chama kimejipanga kutatua uhaba wa maji kwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na kumalizia ujenzi bwawa la Farkwa kusaidia kuleta maji Dodoma.
“Umeme wakati mwingine ni mdogo, tumejipanga kujenga njia kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma ili tupate umeme mkubwa wa kilovoti 400. Tuifanye Dodoma iwe ya viwanda, kazi zote zisisimame kwa sababu ya umeme,” alieleza.
Vilevile, alitoa ahadi ya kuongeza kasi ya upimaji na usajili ardhi ili kutatua migogoro, kukamilisha ujenzi wa kiwanja kikubwa cha mpira wa miguu ambapo tayari mkandarasi ameshapatikana.
Akiwa wilayani Chemba, Rais Dk. Samia alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma ikiwemo barabara ya Chemba – Soya yenye urefu wa kilometa 32.
Alieleza kuwa barabara hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu, hivyo ahadi yake ni kwamba inaenda kutengenezwa kwa kiwango ambacho itakuwa inapitika msimu wote.
“Barabara hiyo ya Chemba – Soya ni tegemeo kwa shughuli za minada inayofanyika kila Jumapili ambayo inaingiza kiasi kikubwa cha fedha ndani ya halmashauri lakini na wafanyabiashara wadogo na wafugaji wanaitegemea kwa kiuchumi,” alieleza.
Akizungumza barabara ya Kwamotoro – Mpende – Kasakai – Ilahoda na zingine tatu za ndani ya wilaya hiyo, aliahidi kuangalia uwezekano Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) kuiboresha ili itumike katika kipindi chote.
Pia, alisema ipo barabara ya Tanga – Handeni – Kiberashi ambayo wamemaliza upembuzi yakinifu na utekelezaji wake utaanza mwaka huu huku akisisitiza barabara hiyo inakwenda kujengwa.
“Lakini kuna ahadi nyingine aliyoitoa mpendwa wetu Dk. Magufuli ya kujenga soko na stendi ndani ya Mji wa Chemba, hii nayo tunakwenda kuifanyia kazi kuhakikisha tunamaliza adha hii ya soko na stendi. Kwa upande wa ujenzi wa bwawa la Farkwa unaendelea vizuri nasi tutaendelea kuhakikisha linamalizika.
“Kwasababu tunalitegemea kwa Mji wa Dodoma ambao sasa ni mji mkubwa wa nchi yetu, uhamiaji umeongezeka, mahitaji ya maji ni makubwa mno. Bwawa kama hili ndilo litakalotuokoa, tutahakikisha linamalizika ili tupate maji ya kutosha ndani ya Mji wa Dodoma,” alibainisha.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe, Dk. Samia aliahidi kuendelea kufanya makubwa zaidi katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu huku akitangaza mpango wa maboresho ya barabara ya TANZAM na reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) lengo likiwa kumaliza msongamano wa maroli yanayokwenda nchini Zambia kupitia mpaka wa Tunduma.
Alisema barabara hiyo imeanza kujengwa kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilometa 75 hatua ambayo itaimarisha shughuli za usafirishaji mizigo katika njia hiyo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe, Dk. Samia alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yamechochea ongezeko la mizigo kutoka tani milioni 15 hadi tani milioni 28 kwa mwaka.
“Natambua maboresho makubwa yaliyofanyika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza mizigo inayotoka nchini kwenda nje ya nchi. Kabla ya maboresho tani za mizigo iliyokuwa ikiingia bandarini ilikuwa milioni 15.8 lakini baada ya maboresho bandari inapokea tani milioni 28 za mizigo.
Alibainisha: “Mzigo unaovuka mpaka wa Tunduma umepanda kutoka tani milioni 3.7 hadi tani milioni tisa. Hali hiyo inaleta msongamano wa maroli ya mizigo yanayoelekea kuvuka mpaka wa Tunduma, kwa maana hiyo tumeanza ukarabati kwa kupanua barabara kuu ya TANZAM inayounganisha Tanzania na Zambia. Kazi inaendelea na tutaendelea nayo mpaka itakapokamilika.”
Dk. Samia alisema ukarabati huo umeanza kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma kwa urefu wa kilometa 75 huku mazungumzo ya kukarabati na kuimarisha reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) yakiendelea.
Alisema reli hiyo ya muda mrefu imechoka na kusababisha kubeba kiwango kidogo cha mizigo wakati huu ambao idadi ya mizigo ikiongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tutakamilisha ujenzi wa Bandari kavu eneo la ekari 1,800 eneo la Katenjele, Kata ya Mpemba ili maroli yasipaki barabarani, tutaongeza barabara ya mbadala itakayoanzia Mwakabanga, tutajenga maegesho ya kisasa, kuongeza mizani, kuharakisha uchakataji nyaraka kabla ya magari kufika mpakani. Pia, serikali tumeanza kuzungumza na mamlaka za ukusanyaji mapato Zambia zifanyekazi saa 24 kama ilivyo kwa Tanzania,” alisisitiza.
Rais Dk. Samia alisema serikali imejipanga kutekeleza mradi wa umeme kutoka Iringa – Njombe hadi Tunduma yenye msongo wa kilovoti 730 ambapo kati ya hizo kilovoti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa huku kilovoti 330 zitakwenda kuuzwa nchini Zambia.
“Tumeshakamilisha mazungumzo, tumeanza mchakato kujenga njia hii ili umeme ufike kwa uhakika. Hii inakwenda sambamba na uhamasishaji matumizi ya nishati safi kwa sababu umeme pamoja na gesi ni nishati safi,” alieleza.
“Nataka kuwathibitishia na kuwaahidi, nitaendelea kufanya makubwa katika sekta ya elimu, afya, maji na umeme. Tunakwenda kutoa huduma kwa wananchi, tutaendelea kuongeza shule, elimu bila ada, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na VETA, kujenga vyuo vya VETA ili kuwawezesha vijana wapate ujuzi na kujiajiri.
Aliongeza: “Tutaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati, tunakwenda kumaliza miradi ya maji lengo kuhakikisha kila Mtanzania apate maji safi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini. Baadhi ya maeneo tumefikia lakini baadhi ya maeneo miradi inaendelea. Umeme tumemaliza vijiji vyote, tupo nusu ya vitongoji na tunakwenda kuunga umeme kila mwananchi afaidike.”
Vilevile, alisema wakati akitoa ahadi kwa mambo atakayoyatekeleza ndani ya siku 100 endapo atakapochaguliwa, alisema mpango wa bima ya afya kwa wote utakaoanza kwa majaribio, wagonjwa watakaopata msamaha wa vipimo vya matibabu ni wale wanaotoka katika kaya masikini.
Mgombea huyo wa Urais kupitia CCM alitumia fursa hiyo kuomba kura kwa wananchi ifikapo Oktoba 29 mwaka huu, wajitokeze kuwapigia kura wagombea wa CCM kuanzia Rais, wabunge na madiwani.
“Kubwa zaidi CCM tunaweza, tunafanyakazi, kujali utu wa mtu na ndiyo maana tunasema ‘Kazi na Utu’ kuanzia huduma za afya, maji ni kujali utu wa mtu, tunapoongeza uzalishaji chakula ni kujali utu wa mtu. lakini la pili tunajiamini, uwezo tunao na nyezo za kufanyiakazi tunazo. Pigeni kura kwa CCM kama kawaida yetu ni mafiga matatu, Rais, wabunge na madiwani,” alieleza.
Akiwa katika mkutano wake uliofanyika viwanja vya TACRI eneo la Vwawa, Dk. Samia alisema serikali imeitendea haki Songwe kwani wabunge wanajivunia maendeleo yaliyofanyikiwa.
“Maendeleo ni tele kwa tele, kuhusu ujenzi wa barabara Mlowo – Kasamba inakwenda kujengwa. Kuhusu mbolea Nilikuwa nazungumza na Waziri wa kilimo, mbolea ya kupandia tumbaku imeshaingia bado kusambazwa, mbolea ya kupandia mazao imeshaingia bado kusambazwa. Niwahakikishie wakulima kwamba mbolea imeingia bado kusambazwa,” alibainisha.
Katika kuboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe, mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga njia ya umeme yenye msongo wa kilovoti 730 itakayokwenda kuimarisha upatikanaji nishati hiyo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano huo, Dk. Samia alisema umeme huo pia utauzwa nchini Zambia.
“Serikali imejipanga kutekeleza mradi wa umeme kutoka Iringa – Njombe hadi Tunduma yenye msongo wa kilovoti 730, kati ya hizo kilovoti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa huku kilovoti 330 zitakwenda kuuzwa nchini Zambia.
Alieleza: “Tumeshakamilisha mazungumzo, tumeanza mchakato kujenga njia hii ili umeme ufike kwa uhakika. Hii inakwenda sambamba na uhamasishaji matumizi ya nishati safi kwa sababu umeme pamoja na gesi ni nishati safi,” alieleza.
Dk. Samia aliongeza: “Nataka kuwathibitishia na kuwaahidi, nitaendelea kufanya makubwa katika sekta ya elimu, afya, maji na umeme. Tunakwenda kutoa huduma kwa wananchi, tutaendelea kuongeza shule, elimu bila ada, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo na VETA, kujenga vyuo vya VETA kuwawezesha vijana wapate ujuzi na kujiajiri.
Akizungumzia miradi ya maji, alisema serikali yake itahakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama kama ilivyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi.
“Tutaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati, tunakwenda kumaliza miradi ya maji lengo kuhakikisha kila Mtanzania apate maji safi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini. Baadhi ya maeneo tumefikia lakini baadhi ya maeneo miradi inaendelea. Umeme tumemaliza vijiji vyote, tupo nusu ya vitongoji na tunakwenda kuunga umeme kila mwananchi afaidike,” alibainisha.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ametoa sh. bilioni 28 kuboresha sekta ya elimu ya msingi na sekondari ikiwemo ujenzi wa shule mpya saba za ghorofa.
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea Ubunge Jimbo la Tunduma, David Silinde alisema miongoni mwa shule zilizojengwa ni shule ya mfano ya Dk. Samia ambayo imejengwa kwa sh. bilioni sita.
Kwa upande wa afya, alisema jimbo hilo lilikuwa na kituo kimoja cha afya cha Tunduma lakini sasa kuna vituo vitano ambavyo vyote vinafanya kazi.
Alieleza kuwa Rais Dk. Samia ametoa sh. bilioni 9.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
“Katika barabara za ndani kulikuwa na mtandao wa kilometa 1.7 lakini kwa sasa zipo kilometa 10.7 ambazo zimejengwa kwa sh. bilioni 5.6. Mikopo ya vijana, wanawake na wazee, Rais Samia ametupatia sh. bilioni 8.1,” alisisitiza.
Kuhusu vyanzo vya mapato, alisema wakati Dk. Samia anaingia madarakani walikuwa wanaingiza sh. bilioni 4.8 lakini sasa wanakusanya sh. bilioni 22.8 huku sekta ya maji wanatekeleza miradi nane yenye thamani ya sh. bilioni 5.1 ambapo mahitaji yalikuwa lita milioni nane lakini kupitia mradi huo watapata lita milioni 20.
Kwa upande wake, mgombea Ubunge Jimbo la Momba, Condester Sichalwe, alimuomba Rais Dk. Samia awapatie kituo cha forodha ili mapato ya ndani katika halmashauri yaweze kuongezeka.
“Miaka minne nyuma tulikuwa tunakusanya sh. bilioni 1.1 lakini kwa sasa tunakusanya sh. bilioni 3.5, tunaamini tukipata geti hata ile mikopo ya asilimia 10 tutaweza kulipa,” alisema.
Condester alisema maendeleo aliyopelekwa katika Jimbo la Momba katika kipindi cha miaka minne ni sawa na fedha zilizotolewa katika miaka 10 iliyopita kwani wamefanikiwa kujenga madarasa 107 katika shule za msingi na madarasa 109 katika shule za sekondari.
Alisema katika sekta ya maji kabla ya miaka minne ya Rais Dk. Samia walipokea sh. bilioni tatu lakini kwa sasa wamepatiwa sh. bilioni 21.6.
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Daniel Chongolo alisema hakuna sababu ya kubishana na wale ambao wanaendeleza maeneo ya uongo kwani ndiyo kazi ambayo watu hao wameichagua.
“Rais wetu anafanyakazi ya ‘katapila’ wapo mabingwa wa kupiga porojo, tuwaachie hiyo ndiyo kazi waliyochagua. Tunapoteza muda na watu waliotimiza wajibu wao, sisi tuna wajibu wa kujenga nchi. Hapa wapo watumishi wa umma kwa kipindi kifupi Rais wetu ameruhusu watumishi wote wenye sifa kupandishwa madaraja,” alieleza.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Tanzania (UVCCM) Mohammed Kawaida, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kutoa ajira kwa vijana, mikopo ya elimu ya juu, vyuo vya kati na mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Kwa upande wake, mgombea Ubunge Jimbo la Vwawa, Japhet Hasunga, alisema ruzuku ya pembejeo iliyotolewa na serikali imewezesha kuongeza uzalishaji chakula hali ambayo imechangia kuongeza kipato cha wananchi hivyo kuwaepusha na njaa.
Pia, alisema zaidi ya sh. bilioni tatu zimetengwa kujengwa soko la kimataifa katika eneo hilo huku sh. bilioni 12.9 zilitolewa kujenga Hospitali ya Rufaa Mkoa ambayo sasa wananchi wanaendelea kupatiwa matibabu.
Vilevile, alisema Rais Dk. Samia alitoa sh. bilioni 3.5 kujenga majengo ya halmashauri katika eneo la Old Vwawa ambako ujenzi unaendeleo.
“Umetupatia sh. bilioni 6.5 kujenga chuo cha VETA Mkoa wa Songwe, ujenzi unaendelea na vijana wanajiandaa kuanza kusoma. Kuna eneo lilitengwa kujenga kituo cha ukaguzi mizigo ambapo kwa miaka 13 wananchi walikuwa wanadai fidia, lakini umeleta fedha sh. bilioni 4.8 wananchi wote wamelipwa fidia,” alisisitiza huku akishangiliwa katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Rodwell Mwampashi, alimshukuru Rais Dk. Samia na Kamati Kuu ya CCM kwa kuwarudisha wabunge waliofanyakazi vizuri katika kipindi kilichopita.
Alisema CCM ilisimamia vyema utekelezaji wa ilani kuhakikisha Ilani ya Chama inatekelezwa kwa usahihi huku akitoa wito kwa wananchi na wanachama wa CCM kumpigia kura Rais Dk. Samia ili aendeleze kasi ya maendeleo mkoani hapa.
Mgombea ubunge Viti Maalum, Juliana Shonza alimpongeza Dk. Samia kwa kuunganishwa mkoa huo katika gridi ya Taifa ya umeme hali ambayo imewafanya kupata nishati hiyo kwa uhakika.
Alisema vitongoji 800 vimeunganishwa na umeme ambapo vimebaki vitongoji 500 ambavyo tayari katika bajeti vitafikiwa.