Arusha, 6 Septemba 2025.
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wamezindua rasmi awamu ya pili ya programu ya Learning for Life katika tawi la NCT Arusha, wakitanua ushirikiano ulioanzishwa jijini Dar es Salaam tangu Septemba 2024.
Kupitia udahili huu wa Arusha, zaidi ya vijana 150 wataandikishwa na kupata mafunzo ya vitendo yanayolenga moja kwa moja ajira katika hoteli za kifahari na za kawaida, migahawa na baa za kanda ya kaskazini ya utalii.
Awamu hii inafuatia mafanikio ya kundi la kwanza lililohitimu Dar es Salaam mwezi Mei 2025, ambapo wanafunzi 100 walifuzu. Utekelezaji wa Arusha umebuniwa kuwa endelevu, huku SBL ikiwekeza katika mfumo wa kuwajengea uwezo wakufunzi wa NCT kupitia Training of Trainers (ToT). Hatua hiyo inalenga kukiwezesha chuo kuendesha makundi yajayo kwa uhuru na uimara, na kuhakikisha upatikanaji wa vijana wenye ujuzi kwa sekta ya ukarimu na utalii – sekta muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.
Programu ya Learning for Life inachanganya darasa la nadharia na mafunzo ya vitendo kazini. Aidha, wanafunzi watanufaika na mafunzo kutoka Diageo Bar Academy kuhusu uendeshaji wa baa, uandaaji wa vinywaji, huduma kwa wateja, pamoja na stadi muhimu za maisha kama mawasiliano, kujenga taswira ya kitaaluma na uongozi. Hatua hii inalenga kuzalisha vijana waliokamilika kitaaluma na kijamii, tayari kuboresha viwango vya huduma na kuongeza ubora wa uzoefu kwa wageni kuanzia siku ya kwanza ya ajira.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey, alisema:
“Programu hii imefungua milango mipya kwa wanafunzi wetu. Inawapa zaidi ya nadharia darasani kwa kuwapeleka kwenye mazingira halisi ya kazi, jambo linaloongeza kujiamini na kuwapa uwezo wa kukidhi matarajio ya waajiri katika sekta ya ukarimu na utalii. Tunajivunia kuendeleza ushirikiano huu na SBL hapa Arusha.”
Mafunzo ya muda mfupi chini ya programu hiyo yanatarajiwa kuanza tarehe 22 Septemba 2025 na kuhitimishwa tarehe 2 Novemba 2025. Gharama zote za mafunzo zitagharamiwa na Serengeti Breweries Limited (SBL), huku wanafunzi wakijigharamia malazi, chakula na usafiri.
Waombaji wanatakiwa kuwasilisha fomu za maombi kabla ya tarehe 16 Agosti 2025. Fomu zinapatikana kupitia tovuti ya NCT (www.nct.ac.tz) au katika ofisi za kampasi za NCT zilizopo Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Sifa za mwombaji ni pamoja na:
Awe Mtanzania.
Awe na barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa/Kijiji au mwajiri.
Awe na umri kati ya miaka 15 – 35.
Awe mwenye afya njema. Awe na elimu ya Cheti au zaidi katika fani ya Ukarimu na Utalii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mauzo wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Bw. Christopher Gitau, alisema:
“Sisi kama SBL tunaamini kwamba kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza kwenye mustakabali wa jamii zetu. Kupitia Learning for Life tunawapa stadi za kiufundi lakini pia tunawajengea uwezo wa kuwa viongozi, wajasiriamali na wachangiaji wakuu wa ukuaji wa sekta ya ukarimu na utalii nchini.”
Programu ya Learning for Life ni sehemu ya ajenda ya kijamii ya SBL iitwayo Spirit of Progress, ikidhihirisha dhamira yake ya muda mrefu ya kuwekeza kwa jamii, kujenga uwezo na kuwawezesha vijana wa Kitanzania. Kupitia upanuzi huu Arusha, programu hii inatarajiwa kutoa fursa mpya za ajira na kuimarisha zaidi sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania.