Maelfu ya wananchi wamejitokeza kumlaki mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mji wa Makambako Septemba 06, 2025 ambako amewahutubia na kuwaomba kura ndiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29,2025 nchini kote.
Festo Sanga Mbunge wa jimbo la Makete akizungumza na Fullshangwe katika mahojiano maalum na kumuelezea Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kiongozi anayekubalika kutokana utendaji kazi wake mahojiano ambayo yamefanyika kando ya mkutano wa kampeni za CCM katika mji wa Makambako.
……………..
NA JOHN BUKUKU MAKAMBAKO
Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga, amesema maelfu ya wananchi waliojitoa kwa wingi kumlaki Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano uliofanyika Makambako ni ishara tosha kuwa wananchi wana imani kubwa na kiongozi huyo kutokana na utendaji wake wa kazi katika kipindi cha miaka minne akiwa madarakani.
Sanga ameyasema hayo katika mahojiano maalum na mtandao wa Fullshangweblog kando ya Mkutano wa Kampeni wa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika katika mji wa Makambako akiwa njiani kuelekea mkoani Iringa kuendelea kampeni zake.
Amesema, “Hiki chama ni kikubwa na unaweza kuona namna watu walivyojitokeza hapa Makambako kwa ajili ya kumpokea Mheshimiwa Rais. Umati huu na maelfu ya watu waliokusanyika ni uthibitisho kuwa wananchi wana imani na Rais Samia. Haya hayatokei kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya kazi nzuri alizofanya.”
Aidha, Sanga aliongeza kuwa wananchi walionekana na shauku kubwa huku wakiendesha shamrashamra za kumshukuru na kuonyesha kumuunga mkono Rais Samia kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, akisisitiza kuwa Wananjombe na wananchi wa Makambako wako tayari kuhakikisha ushindi wa CCM.
Akizungumzia hali ya bunge, alisema: “Wakati naingia bungeni moja ya mambo yaliyozungumzwa ni kuwa nusu ya bunge hubadilika kila baada ya uchaguzi. Asilimia 50 hadi 60 ya wabunge huanguka, na hili nimeliona. Hata hivyo, tunatarajia kuwa bunge lijalo litakuwa la moto na litakuwa msaada mkubwa kwa Taifa letu.”
Sanga alisisitiza kuwa wabunge wanapaswa kuhakikisha wanashawishi na kusimamia maslahi ya Watanzania. Alibainisha kuwa amekuwa akiamini kuwa Mungu ndiye chanzo cha yeye kuwa mbunge, lakini pia ni matokeo ya kazi aliyofanya kwa wananchi.
“Watanzania wamebadilika, leo hii unaweza kuwapa hela wakapokea lakini kura hawakupi kama hufanyi kazi. Mimi nimeshinda kwa sababu nilifanya kazi, wananchi walinipa nafasi kwa miaka mitatu iliyopita na walinihakikishia 2025 watanichagua tena, na kweli ndivyo ilivyokuwa,” alisema.
Mbunge huyo alihitimisha kwa kusema kuwa wananchi sasa wanachagua viongozi wanaofanya kazi, na kwamba kila aliyepewa nafasi anatakiwa kuitendea haki. Vinginevyo, alisema, chama kinaweza kuathirika. Pia, alisisitiza umuhimu wa vijana kuaminika katika nafasi za uongozi kwa manufaa ya Taifa.
Wabunge wa. mkoa wa Njombe wakiwa katika mkutano wa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Makambako.
Msafara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ukiwasili katika mji wa Makambakomkoani Njombe ambako kumefanyika mkutano wa kampeni kabla ya kuendelea na kampeni zake kuelekea mkoani Iringa.