Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waumini wa dini ya kiislam alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika baraza la Maulid Kitaifa linalofanyika, Korogwe mkoani Tanga, Septemba 05, 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin in Ali na Mama Shamim Khan, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika baraza la Maulid Kitaifa linalofanyika, Korogwe mkoani Tanga, Septemba 05, 2025
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana ma waumini wa dini ya kiislam baada ya kuhutubia baraza la Maulid Kitaifa linalofanyika, Korogwe mkoani Tanga, Septemba 05, 2025 kwa niana ya Rais Samia Suluhu Hassan. kushoto ni Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin in Ali
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin in Ali ya kutambua mchango wake katika kuendeleza dini ya kiislam. Tuzo hiyo imetolewa na BAKWATA.
…………
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania imejengwa kwa misingi imara ya amani, uzalendo na maadili mema ambayo yameasisiwa na viongozi wa Taifa hilo.
Amesema kuwa wakati wote viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali kuhamasisha amani, kukemea uovu na utovu wa nidhamu katika jamii ili kujenga kizazi chenye heshima, mshikamano na uzalendo kwa Taifa.
Amesema hayo leo Ijumaa (Septemba 05, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika Wilayani Korogwe mkoani mkoani Tanga.
Amesema kuwa Maulid ni tukio lililobeba mwongozo wa kiroho kwa wanadamu wote. “Maisha ya Mtume yanaonesha mfano na yanatufundisha kuwa waadilifu, kuishi kwa maadili, na kumtegemea Mwenyezi Mungu. katika kila jambo”. Amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin Ali ametoa wito kwa Masheikh nchini kuendelea kuhubiri amani katika maeneo yao kwa kuwa amani si jambo la hiari hivyo kila mmoja anapaswa kusimamia uwepo wake. “Wafundisheni waumini katika majukwaa yenu ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, kemeeni vitendo vyote vyenye ishara ya uvunjifu wa amani”
Akisoma salam za Baraza kwenye sherehe za baraza la maulid, Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaj Nuhu Jabir Mruma amesema kuwa amani na utulivu ni kigezo kikuu cha maendeleo kwa bila amani hakuna Ibada, hakuna maisha wala maendeleo yoyote.
“Hali kubwa ya maendeleo tuliyonayo na yanayoshamiri leo katika nchi yetu msingi wake mkubwa ni amani. Hatuna budi Watanzania wote kuienzi TUNU ya amani tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kupitia jukwaa hili tunawanasihi Waislamu na wananchi kwa ujumla kuzingatia misingi ya amani na utulivu katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025”.