NA JOHN BUKUKU – NJOMBE
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wagombea wote waliofanikiwa na hata wale ambao hawakufanikiwa katika kura za maoni, kuungana pamoja na kuvunja makundi ndani ya chama.
Dkt. Samia alitoa wito huo alipohutubia wananchi wa Mkoa wa Njombe waliojitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Njombe.
Amesema ni jambo la msingi sana kwa wakati huu wanachama wa CCM kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja, ili chama kiingie kwenye uchaguzi kikiwa na mshikamano na nguvu kubwa.
“Nampongeza Mwenyekiti wa Mkoa, Deo Sanga, na niungane naye katika jambo la kuvunja makundi. Nimpongeze sana kwa hatua hii,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza: “Niwaombe sana wagombea wote waliofanikiwa na ambao hawakufanikiwa, tuvunje makundi turudi kuwa chama kimoja ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa na nguvu kubwa.”
Dkt. Samia amesema mshikamano wa ndani ya chama ndio nguzo kubwa ya ushindi, hivyo kila mwanachama anapaswa kuweka mbele maslahi ya chama na taifa badala ya makundi binafsi.
Rais Samia amewaomba wananchi wa Njombe kumpigia kura zote za ndiyo na kuwapigia wabunge wa CCM na Madiwani wa CCM itakapofika Oktoba 29,2025 ili serikali iweze kutekeleza kwa ufanisi miradi na kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga, amesisitiza kuwa chama kinapokuwa na mshikano imara, kitakuwa na uwezo mkubwa wa kushinda uchaguzi na kuendelea kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.