Na Mwandishi, Dodoma
KAMAPUNI ya Oryx Gas Tanzania imetoamitungi ya gesi 260 kwa Chama Cha Skauti Tanzania ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ifikapo mwaka 2030.
Hayo yalibainishwa jijini hapa jana na Meneja Mauzo Oryx Tanzania Bara, Alex Wambi wakati wa ufunguzi wa kambi ya kielimu ya Skauti Taifa inayofanyoka katika viwanja vya Don Bosco.
“Kampuni inatoa mitungi na majiko ya gesi 260, makubwa na madogoi, kwa Chama cha Skauti Tanzania na kwamba mchango huo si gesi tu bali ishara ya imani, maadili ya pamoja, na dhamira ya kujenga mustakabali salama na wenye matumaini.
Aliongeza kuwa :”Sababu ya Oryx Gas kutoa mitungi hiyo ni kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi na usalama kuanzia ngazi ya familia, shule, na jamii kote Tanzania,”alisema
Katika hatuaa nyingine alisema kambi hiyo ni darasa hai hivyo Skauti watajifunza jinsi ya kutumia gesi ya LPG kwa usalama, kuelewa faida zake, na kuwa mabalozi wa nishati safi katika maeneo yao.
Wambi alisema mbali na vifaa vya LPG, Oryx Gas pia itaendesha vipindi vya elimu kuhusu usalama, ufanisi wa nishati, na mchango wa kupikia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka wizara ya Nishati Nolasco Mlay alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia ili kuepuka madhara yatokanayo na nishati isiyofaa.
Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia husaidia kuokoa muda wakati wa kupika na kuzuia ukataji miti hovyo kwa ajili ya kuni na kuchoma mkaa.
“Matumizi ya nishati yasiyofaa yanaathali kubwa kiafya na kimazingira.Lengo la serikali nikuona wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuepuka madhara hayo.
Awali Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Victor Bundikwi aliwasisitiza Chama cha skauti Tanzania kuendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kutunza amani na utulivu.
Pia aliwasisitiza kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi bora katika uchaguzi unaotarajia kufanyika 28 Oktoba mwaka huu.
Vilevile aliwataka vijana wa Skauti Tanzania kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kujnga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.