Imeandikwa na Alex Msama Mwita.
SHALOM!
BINAFSI, ni buheri wa afya njema.
Hakika ninamshukuru mno Mungu wa Mbinguni, kwa kuendelea kunilinda, mimi na familia yangu, lakini zaidi sana kwa kuendelea kusimamia Amani na utulivu kwa nchi yangu niipendayo, Tanzania.
Ninaendelea kumuomba Mungu azidi kusimama nasi, kama Watanzania katika kudumisha umoja, ushirikiano, mshikamano na undugu wetu, tuliorithishwa na waasisi wa Taifa letu.
Ndugu zangu, saa chache zilizopita, kulisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, juu ya kile kinachotajwa kuwa orodha ya wagombea wa nafasi ya ubunge, katika majimbo mbalimbali hapa nchini, kupitia chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA).
katika hali ya kushangaza, kushtusha, kuduwaza na kuacha maswali mengi, ni pale nilipoona jina langu, kuwa miongoni mwa wagombea hao wa ubunge, nikitajwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Ukonga!
Ndugu zangu, nichukue nafasi hii kuonesha masikitiko yangu makubwa sana, juu ya jambo hili!
Sihusiki, sijahusishwa na wala sijui chochote kuhusu orodha hiyo na nimesikitika mno, jina langu kuwa sehemu ya orodha hiyo ambayo binafsi siitambui kwa namna yoyote!
Nipende kuwajulisha Watanzania wenzangu, wanachama wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwamba sijafanya uamuzi wowote unaohusisha kuhama chama changu pendwa, CCM, wala kujiunga na chama chochote cha siasa, nje ya CCM!
Niwaondoe hofu na wasiwasi watu wangu wa karibu, wanachama wenzangu wa CCM, ndugu na marafiki, muhimu zaidi, viongozi wangu wa CCM, kuanzia ngazi ya Taifa hadi shina, mimi Alex Msama, sihusiki kwa namna yoyote ile na Chauma.
Jambo hili limezua taharuki kubwa, kwa familia yangu, rafiki, ndugu na watu wangu wa karibu, simu zimekuwa nyingi sana, wakitaka uhakiki na uthibitisho wa walichokiona!
Mimi Alex Msama Mwita, siyo tu kwamba sijahama CCM, bali sijawahi kuwaza, kufikiria, kudhani na wala kuota kuondoka CCM.
Bado na nitabaki kuwa mwachama mtiifu wa CCM, nikiendelea kuunga mkono jitihada na kazi kubwa inayofanywa na CCM, katika kuwahudumia Watanzania.
Hakika NINALAANI VIKALI mno, upotoshaji na uzushi huu, ambao siyo tu kwamba umeleta usumbufu, bali pia umenipa maumivu makali ya moyo na hisia, mimi binafsi na watu wangu wa karibu, hususan familia yangu!
Bado ninafanya uchunguzi wa kina, mimi na timu yangu, wakiwemo wasaidizi wangu wa masuala ya kisheria, ili kubaini kama kweli orodha hii imeandaliwa na CHAUMA, ili hatua kali za kisheria zichukue mkondo wake.
Kwa sasa niwaombe na kuwataka Watanzania, wanachama wenzangu wa CCM na watu wangu wote wa karibu, wapuuzie uzushi, uvumi na upotoshaji huo!
Kama nilivyobainisha hapo juu, uchunguzi ukikamilika nitakuja na tamko rasmi juu ya hatua stahiki itakayofuata.
Kwa sasa niombe utulivu juu ya jambo hili na kwamba lipo kwenye hatua nzuri, katika kulishughulikia.
Kwa sasa tuelekeze akili, utashi, nguvu, sala, maombi na dua zetu katika Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mnamo Oktoba 29, mwaka huu.
Tuwaombee afya njema wagombea wote wa nafasi mbalimbali, huku tukiunga mkono sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tumuunge mkono Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombe Mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, wabunge na madiwani wote wa CCM.
Nihitimishe waraka huu kwa kuwahakikishia tena Watanzania kuwa, mimi Alex Msama, sijajiunga na chama chochote cha siasa, zaidi ya kuendelea kuwa mwanachama halisi wa CCM.
Hata hivyo, niwaombe viongozi wa CHAUMA, kutoa ushirikiano wowote nitakaouhitaji katika uchunguzi wa sakata hili.
Wenu katika Ujenzi wa Taifa,
Alex Msama,
Mkurugenzi Mtendaji – Msama Promotions.