Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni zake Jiji la Mbeya tarehe 04 Septemba, 2025 katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Mbeya.
Spika wa Bunge na Mgombea Ubunge Jimbo la Uyole jijini Mbeya, Dkt. Tulia Ackson akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea nafasi ya urais kupitia tiketi ya CCM uliofanyika kwenye uwanja wa Airport ya zamani jijini Mbeya Septemba 04, 2025.
…………..
NA JOHN BUKUKU – MBEYA
Spika wa Bunge na Mgombea Ubunge Jimbo la Uyole jijini Mbeya, Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa wananchi wa Mbeya hawana sababu ya kumnyima kura Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika jiji hilo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Dkt. Samia uliofanyika Septemba 4, 2025 kwenye uwanja wa Airport ya zamani jijini Mbeya, Dkt. Tulia alisema miradi iliyotekelezwa katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi ni kielelezo cha dhahiri cha uongozi bora wa Rais Samia.
Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, katika sekta ya afya zaidi ya shilingi bilioni 20 zimetolewa, ambapo Hospitali ya Meta imenufaika kwa kupata shilingi bilioni 11. Aidha, vituo vya afya katika kata za Iyela, Itagano na Mwakibete vimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 kila kimoja.
“Hospitali ya Rufaa ya Kanda sasa inatoa huduma za vifaa tiba vilivyokuwa vinapatikana Dar es Salaam pekee, jambo linalorahisisha huduma kwa wananchi wetu wa Mbeya na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,” alisema.
Akizungumzia sekta ya elimu, Dkt. Tulia alisema zaidi ya shilingi bilioni 31.1 zimetumika kujenga shule mpya za msingi na sekondari. Miongoni mwa shule hizo ni Bombambili (Kata ya Mwakibete), Sekondari ya Sewa na Sekondari ya Airport. Shule mpya ya msingi pia imejengwa katika Kata ya Ilemi na kupewa jina la Chifu Rocket Mwashinga kama heshima ya mchango wake kwa jiji la Mbeya. Aidha, shule ya msingi na sekondari zimejengwa Itagano, hatua iliyoondoa changamoto ya wanafunzi kutembea mwendo mrefu kufuata elimu ya sekondari.
Kwa upande wa maji, alisema shilingi bilioni 30 zimetumika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, ambapo kata nyingi kati ya 36 za Mbeya Mjini sasa zimeunganishwa na maji safi. Pia, alibainisha kuwa Mradi mkubwa wa Maji wa Kiwira unatarajiwa kumaliza kabisa tatizo la maji katika jiji la Mbeya na maeneo ya jirani.
Aidha, alitaja utekelezaji wa mradi wa TACTIC ulioleta ujenzi wa stendi ya mabasi ya mkoa yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 21.7, pamoja na ujenzi wa soko jipya la kisasa katika Kata ya Maendeleo (Sokomatola) litakalogharimu zaidi ya shilingi bilioni 6.
Kuhusu barabara, Dkt. Tulia alisema barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 imeanza kutekelezwa, ambapo awamu ya kwanza ya kilomita 29 kutoka Uyole hadi Ifisi imeshakamilika. Pia, barabara ya njia panda ya Airport yenye kilomita tatu imepangwa kupandishwa hadhi kuwa njia nne.
Kwa upande wa uwezeshaji wananchi, Dkt. Tulia alisema zaidi ya wananchi 3,000 wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wamenufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais kuhusu asilimia 10 ya mapato hayo.
“Kwa miradi hii mikubwa tuliyoshuhudia, hatuna sababu ya kumnyima kura Dkt. Samia. Amefanya mambo makubwa kwa wananchi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla, na sasa ni jukumu letu kumrudishia heshima kwa kumpa kura za ushindi,” alisema Dkt. Tulia.
Alisisitiza kuwa wananchi wa Mbeya wanapaswa kuungana kwa mshikamano wa dhati na kuhakikisha kura zote za urais zinamwendea Dkt. Samia ili aendelee kuongoza taifa na kukamilisha miradi ya maendeleo aliyoiweka katika Ilani ya CCM 2025–2030.