Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mbalizi katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Mbeya tarehe 04 Septemba, 2025.
Pareto Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mlima Reli Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijiji.
…………….
NA JOHN BUKUKU- MBALIZI
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali yake itakapopata ridhaa ya wananchi itaendelea kuboresha sekta ya kilimo hususan zao la pareto ambalo limefufuliwa na kuonekana kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima wa Mbeya Vijijini.
Akizungumza leo Alhamisi, Septemba 4, 2025, katika viwanja vya Mlima Reli Mbalizi mkoani Mbeya wakati akinadi Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025–2030, Dkt. Samia aliwahakikishia wakazi wa wilaya hiyo kuwa juhudi za kuimarisha kilimo zitahusisha mbegu bora, mbolea ya ruzuku, pamoja na pembejeo nyingine ili kuongeza tija kwa wakulima wa pareto na mazao mengine.
“Pareto ni zao lenye faida kubwa kwa wakulima wetu na serikali itahakikisha linaendelea kuchangia kipato cha kaya na taifa kwa ujumla. Nawataka wakulima kuendelea kujisajili kwenye mfumo wa pembejeo ili wanufaike na mbolea na ruzuku zinazotolewa na serikali,” alisema Dkt. Samia.
Mbali na kilimo, aliahidi pia kuboresha huduma muhimu za kijamii zikiwemo afya, maji safi na salama, nishati ya umeme, elimu, pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara ikiwemo ile ya Mbalizi kwenda Mkwajuni. Aidha, alibainisha kuwa serikali itajenga machinjio katika eneo la Utengule na kuimarisha sekta ya mifugo.
Kuhusu maendeleo ya miji, Dkt. Samia alisema ombi la Mbalizi kupandishwa hadhi kuwa mji kamili lipo katika hatua mbalimbali na serikali yake italifanyia kazi ipasavyo.
Awali akizungumza katika mkutano huo kuhusu maboresho ya zao la Pareto Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani kimeleta mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo kufufuliwa kwa zao la pareto ambalo lilikuwa limesahaulika kabisa.
Prof. Kabudi amesema juhudi za Dkt. Samia kwenye kilimo zimekuwa za mfano, hasa kupitia ruzuku na uwekezaji uliofanywa katika zao la pareto.
“Katika kilimo umefanya mambo makubwa sana, ikiwemo kulifufua zao la pareto. Jitihada na ruzuku ulizoweka zimeifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa pareto duniani, ikifuatiwa na Australia, na mafanikio haya yamepatikana ndani ya kipindi cha miaka mitatu tu,” alisema Prof. Kabudi.
Mbali na kilimo, Prof. Kabudi alieleza kuwa Rais Samia ameboresha maisha ya wananchi wa Mbeya kwa kuboresha huduma za afya, maji, na nishati, hatua iliyowapa wananchi uwezo wa kufanya biashara na kuinua hali za maisha ya familia zao.
Akitolea mfano, alisema alipata fursa ya kuzindua kituo cha afya Tukuyu kwa niaba ya Rais Samia, kituo chenye thamani ya shilingi milioni 800 na kukiita cha mfano kutokana na vifaa tiba na wataalamu waliopo.
“Kituo kile kimenishangaza, kwa sababu vifaa vilivyopo pale ni sawa na vile vya hospitali kubwa za kitaifa, utafikiri ni hospitali ya mkoa. Huu ni ushahidi kwamba kazi kubwa imefanyika chini ya uongozi wako,” alisema Prof. Kabudi.
Aidha, alibainisha kuwa changamoto zote zilizowasilishwa na wananchi zimo ndani ya Ilani ya CCM 2025–2030 na kwamba Dkt. Samia ameweka nia ya kuzifanyia kazi kwa vitendo.