NA JOHN BUKUKU – MBEYA
Jiji la Mbeya limevunja rekodi kwa umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye uwanja wa Airport, jijini Mbeya.
Umati wa maelfu ya wananchi umejitokeza kumsikiliza Dkt. Samia, huku wakiashiria imani kubwa waliyonayo kwa sera na mipango ya maendeleo inayosimamiwa na CCM kupitia Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030.
Wananchi hao wameendelea kumuunga mkono kwa wingi, hasa baada ya kutekelezwa kwa miradi mikubwa katika sekta mbalimbali mkoani Mbeya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara ya Tanzam, ukarabati wa reli ya TAZARA, upanuzi wa huduma za Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, miradi ya maji safi vijijini na mjini, pamoja na uwekezaji katika nishati ya umeme. Hatua hizo zimeongeza imani kubwa ya wananchi kwa Dkt. Samia na kuifanya kampeni zake kupata mwitikio mkubwa zaidi.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia amewahimiza wakazi wa Mbeya kuendeleza mshikamano, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, na kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za kijamii na sekta za kiuchumi ikiwemo kilimo, afya, elimu, maji na nishati.
Julieth Mwakalukwa, mkazi wa Sai jijini Mbeya, amesema kuwa miradi ya maji safi na huduma za afya iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi. “Kwa kweli Rais Samia ametufanyia makubwa. Tunapata huduma za afya kwa urahisi na maji yapo karibu, hali ambayo imeboresha maisha yetu,” amesema.
Kwa upande wake, Andusamile Mwakatobe, mkazi wa eneo la Nzovwe alisema mradi wa upanuzi wa barabara utafungua fursa za kibiashara kwa wananchi wa Mbeya na maeneo jirani. “Mawasiliano yakiboreshwa, biashara zetu zinaenda vizuri na uchumi wetu utakua. Hii ndiyo sababu tutamuunga mkono Dkt. Samia kwa kura zetu,” amesema Mwakatobe.
Wananchi waliokuwepo katika mkutano huo walionekana kufurahishwa na hotuba ya mgombea huyo, huku wengi wakiahidi kumpa kura ili aendelee kuongoza taifa na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.