Umati mkubwa wa wananchi wakiwa wamejitokeza kwenye mkutano wa kampeni wa Chama cha Mapinduzi CCM kwenye uwanja wa Mlima Reli Mbalizi wilaya ya Mbeya vijijini ambapo mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM atazungumza na wananchi na kuomba kura za ndiyo ifikapo Oktoba 29, 2025 utakaofanyika nchini Kote
…………
NA JOHN BUKUKU- MBALIZI- MBEYA
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Mbeya Mjini kujitokeza kwa wingi kumlaki na kushiriki katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaotarajiwa kuanza saa sita mchana leo.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Kihongosi alisema maandalizi yamekamilika na shamrashamra zimepamba moto huku wananchi wa Mbeya wakiwa na hamasa kubwa ya kumpokea mgombea huyo.
“Akina baba wanaita Mama, akina mama wanaita Mama na watoto nao wanaita Mama. Hakika Dkt. Samia anatosha. Hata wapinzani nao wanahoji ‘Mama anakuja lini?’ jambo linalothibitisha namna wananchi wote wanavyosubiri kwa shauku kubwa ujio wake,” alisema Kihongosi.
Kihongosi alisisitiza kuwa CCM ni miongoni mwa vyama vikubwa barani Afrika na duniani, jambo linalothibitisha imani kubwa ya wananchi kwa chama hicho.
“Tunajaza mikutano si kwa sababu ya kusomba watu, bali ni kwa mapenzi ya wananchi. Wananchi wanakuja wenyewe kwa sababu ya imani waliyo nayo kwa CCM na kwa kiongozi wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Akizungumzia kazi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia, Kihongosi alisema kila mkoa, wilaya, kata na kijiji kimeguswa na miradi ya maendeleo.
“Sekta ya nishati, kwa mfano, vijiji vyote sasa vimepatiwa umeme. Haya si maneno, bali ni matokeo ya kazi za Dkt. Samia ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, fedha za vijana na wanawake, pamoja na ujenzi wa barabara ni miongoni mwa mambo yaliyotekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Kihongosi alisema kampeni za CCM zinafanyika kwa staha na utu, bila kutumia lugha za matusi au kejeli.
“Tunaenda kuwaambia Watanzania nini tunawaandalia kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030. Tayari Ilani ya 2020/2025 imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 95. Hivyo basi, wananchi wana kila sababu ya kuendelea kuiamini CCM,” alisema.
Aidha, Kihongosi alisisitiza kuwa hakuna mgombea wa vyama vingine anayeweza kulinganisha uwezo wa uongozi wa Dkt. Samia.
“Dkt. Samia ana uzoefu mkubwa ndani ya CCM, ndani ya serikali na hata katika majukwaa ya kimataifa. Hawa wapiganaji wadogo hawana sera madhubuti wala uzoefu wa kuendesha nchi,” alisema.