Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Mgombea urais kupitia Chama Makini, Coster Kibonde, amesema pindi atakapopata ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atampa uongozi wa juu mgombea urais Kupitia tiketi ya CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na umahiri wake katika uongozi.
Akizungumza leo Septemba 2, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, Kibonde alisema Dkt. Samia ni mwanadiplomasia mzuri ambaye amefanya mambo mengi mazuri katika kipindi chake cha uongozi na hayapaswi kubezwa.
“Pindi wananchi watakaponipa ridhaa na Tume Huru kunitangaza kuwa Rais wa nchi hii, viongozi wote waliokuwa kwenye mchakato wa kugombea urais nitawapa nafasi kwenye serikali yangu. Lakini nafasi ya kwanza nitampa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani huyu ni mwanadiplomasia mzuri na ninaamini ataendelea kufanya kazi nzuri kwenye serikali,” alisema Kibonde.
Akieleza vipaumbele vya chama chake endapo kitapata ridhaa ya wananchi, Kibonde alisema wamejikita katika sekta tatu kuu ambazo ni elimu, kilimo na afya.
Kuhusu elimu, alisema wanakusudia kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu. Katika sekta ya afya, alisema watajenga hospitali katika kila kata, kuzipatia vitendea kazi na kutoa fursa kwa madaktari na wauguzi kwenda nje ya nchi kupata uzoefu ambao utatumika kuboresha huduma nchini.
Akizungumzia kilimo, Kibonde alisema chama chake kimejipanga kugawa heka tano kwa kila kijana pamoja na pembejeo, huku wakipewa hati miliki za ardhi hiyo ili waweze kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha.
Kwa upande wake, mgombea mwenza Azza Haji Suleiman, aliwataka vijana kuepuka kutumika kuvunja amani hasa kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
“Vijana niwasihi tudumishe amani na utulivu ili uchaguzi uwe wa amani. Muepuke kushawishiwa kuwa chanzo cha machafuko, kwani mkumbuke pindi amani ikikosekana, wagonjwa, wazee na watoto ndio watakaoathirika zaidi. Niwaombe muendelee kuwa mabalozi wazuri wa amani nchini,” alisema Azza.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye pia ni mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ameir Hassan Ameir, alisema endapo wataingia madarakani wataanzisha mfuko wa mikopo kwa mama lishe bila riba ili kumsaidia mwanamke kuinuka kiuchumi.
Aliongeza kuwa chama hicho pia kitaleta pikipiki (bodaboda) milioni moja bure kwa vijana ili kuchochea ajira, kutoa mikopo ya shilingi milioni 10 kwa wafanyabiashara wa mitumba, pamoja na posho ya shilingi 100,000 kwa mwezi kwa wazee wote nchini.