Na John Bukuku – Songwe
Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema dhana ya uongozi wa kweli ni ile inayoshirikisha chama na wananchi katika kupeleka taifa mbele, akisisitiza kuwa huo ndiyo msingi wa kazi na utu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Septemba 3, 2025 katika viwanja vya Mbimba, Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe, Chongolo alisema:
“Kazi ya kusema ni rahisi, lakini kazi ya kutenda ni ngumu. Inahitaji maarifa, kujitoa, upendo, kujituma, utayari na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi waliokupa dhamana. Ndiyo maana tunasema kazi na utu – tunasonga mbele.”
Chongolo alieleza kuwa Serikali chini ya Rais Samia imekuwa mfano wa uongozi wa vitendo, ambapo watumishi wa umma waliokuwa wakistahili kupandishwa madaraja wamepandishwa kwa wakati, jambo linalodhihirisha uadilifu na dhamira ya kweli.
Akizungumzia sekta ya maji, Chongolo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe amesema Rais Samia amepeleka shilingi bilioni 119 kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Songwe. Akinukuu kauli ya mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduma, David, alisema:
“Maji yanayozalishwa ni lita milioni 20, huku mahitaji yakiwa milioni 8 pekee. Hivyo, lita milioni 12 zinazobaki zitasaidia maeneo ya Ihanda na Mlowo.”
Chongolo aliongeza kuwa CCM ni chama kinachoishi kwa vitendo, kikiongozwa na dhamira ya kuhakikisha wananchi wanakwenda mbele wakiwa salama, na kwamba uongozi wa Dkt. Samia umeweka msingi wa maendeleo unaogusa maisha ya kila Mtanzania.
“Chama kinachotawala lazima kiwe na dhamira ya kweli ya kupeleka wananchi wake mbele. Ndiyo maana CCM na Rais Samia wamesimama imara – wanatekeleza kwa vitendo na si kwa maneno. Hii ndiyo maana halisi ya kazi na utu,” alisisitiza Chongolo.