
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga Meja Jenerali Shaban Baragash Mani (kulia) akimkabidhi bendera ya Taifa Mkuu wa kikundi kinachoenda kushiriki mazoezi ya Jeshi la Anga ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nchini Zambia, Kanali Lazarro Kidendea Bunnus katika hafla iliyofanyika leo Septemba 2, 2025 katika Kikosi cha Anga cha JWTZ, Airwing, jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga Meja Jenerali Shaban Baragash Mani akizungumza katika hafla ya kukabidhi bendera ya Taifa kwa kikundi kinachoenda kushiriki Mazoezi ya Jeshi la Anga ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nchini Zambia iliyofanyika leo Septemba 2, 2025 katika Kikosi cha Anga cha JWTZ, Airwing, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Brigedia Jenerali Zeno Johnson Sikukuu akizungumza katika hafla ya kukabidhi bendera ya Taifa kwa kikundi kinachoenda kushiriki Mazoezi ya Jeshi la Anga ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nchini Zambia iliyofanyika leo Septemba 2, 2025 katika Kikosi cha Anga cha JWTZ, Airwing, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga Meja Jenerali Shaban Baragash Mani akiwa katika picha ya pamoja na kikundi kinachoenda kushiriki mazoezi ya Jeshi la Anga ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nchini Zambia.
Picha za matukio mbalimbali.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajia kushiriki mazoezi ya pamoja ya Jeshi la Anga ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yatakayofanyika nchini Zambia kuanzia Septemba 8 hadi 26, mwaka huu.
Akizungumza leo Septemba 2, 2025, katika hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa kwa kikundi kinachoenda kushiriki mazoezi hayo, iliyofanyika katika Kikosi cha Anga cha JWTZ, Airwing, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Meja Jenerali Shabani Balaghash Mani, amesema mazoezi hayo ni muhimu kwa ajili ya kujiandaa kukabiliana na majanga ya kibinadamu, na kuhakikisha Jumuiya hiyo inabaki salama na imara.
Meja Jenerali Mani amesema ushiriki wa JWTZ katika mazoezi hayo una manufaa makubwa katika nyanja mbalimbali, zikiwemo shughuli za kiulinzi, kiuchumi na kibiashara.
“Ushiriki wa JWTZ utasaidia kupata uzoefu wa namna ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa wenzao wakati wa majanga, hasa katika kuokoa maisha. Majeshi ya anga yana uwezo wa kufika kwa haraka katika maeneo yaliyoathirika na kutoa msaada wa dharura,” amesema Meja Jenerali Mani.
Ameongeza kuwa: “Tutanufaika kwa kufanya mazoezi ya pamoja, kujifunza mbinu mpya kutoka kwa wenzao, kuwashirikisha uzoefu wetu katika shughuli za uokoaji na utoaji wa msaada wakati wa majanga, hata kama kuna tishio la kivita, na pia kujiweka tayari hata katika kipindi cha amani.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Brigedia Jenerali Zeno Johnson Sikukuu, amesema lengo kuu la mazoezi hayo ni kuviandaa vikosi vya anga vya SADC kushirikiana katika operesheni za utoaji wa msaada katika mazingira yenye changamoto, hasa zile zenye tishio la kigaidi.
Brigedia Jenerali Sikukuu ameongeza kuwa msaada wa kibinadamu ni jukumu linalohitaji ushirikiano, mshikamano na weledi wa hali ya juu miongoni mwa majeshi ya nchi wanachama.