Kushoto ni Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Rukwa akimtambulisha mgombea ubunge Jimbo la Sumbawanga kwa wananchi wakati wa ufunguzi wa kampeni.
Baadhi ya wagombea waliotambulishwa kwa wanachama wakati wa ufunguzi wa kampeni
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi ccm mkoa wa Rukwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni zilizofanyika wilayani Nkasi
Mwenyekiti wa chama wakati akimkabidhi mgombea wa Jimbo la Nkasi kaskazini ilani ya chama cha mapinduzi
Baadhi ya wagombea udiwani waliohudhuria ufunguzi wa kampeni hizo
Na Neema Mtuka Nkasi
Rukwa:Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Rukwa kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi, ambapo mgeni rasmi, Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Ashlafu Maufi, amewaomba wananchi kuendelea kukipa ridhaa chama hicho ili kiendelee kushika dola.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Rukwa Ashlafu Maufi amesema kuwa mwanzo huo wa kampeni umefungua ukurasa mpya kwa wagombea kunadi sera za chama chao.
Akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, Maufi amesema (CCM) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na kilimo, jambo linalothibitisha dhamira ya chama hicho katika kuinua maisha ya wananchi.
“Niwaombe wanachama tuendelee kukiamini chama chetu,na kuwa na imani na wagombea wetu kwa ngazi ya urais ubunge na udiwani.”
Amesema maufi.
Awali mwakilishi wa sheikh wa wilaya ya Nkasi Mauridi Issa amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni ili kusikiliza sera za wagombea na kufanya maamuzi sahihi ifikpo oktoba 29.
Aidha amewataka wanasiasa wote kufanya siasa za kistaarabu zisizogawa wananchi kwa misingi ya dini, kabila au itikadi, ili kudumisha amani na mshikamano wa taifa.
“Tufanye kampeni zetu kama ambavyo miongozo inatutaka kufanya tusiwayumbishe wananchi kwa maneno na tusifanye kampeni zenye kuleta uchochezi”. Amesema
Kwa upande wao baadhi ya wanachama walioshiriki katika ufunguzi wa kampeni hiyo akiwemo Sarah Lazaro amewahimiza wananchi na wanachama kushiriki kikamilifu katika kampeni kwa lengo la kusikiliza sera za wagombea na kufanya maamuzi hapo oktoba 29 na kupata viongozi bora watakaoleta maendeleo.
“Tujitokeze kwa wingi tusikilize kampeni za wagombea wetu wote na tuwachague viongozi wenye maadili watakaotuletea maendeleo.”amesema Sarah.
Uzinduzi huo wa kampeni ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na jumuiya zake, pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Rukwa.