Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika mkutano wa hadhara wa Kampeni za Uchaguzi za Chama hicho uliofanyika Chadulu Jijini Dodoma tarehe 31 Agosti, 2025.
Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makamu Wenyeviti Wastaafu mzee Philip Mangula kushoto na Mzee John Samuel Malecela Mara banda ya kuhutubia mkutano wa kampeni jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Balozi Dkt. Bashiru Ali Kakurwa akizungumza katika mkutano huo.
………..
NA JOHN BUKUKU- DODOMA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu katika Mkoa wa Dodoma ni ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu mikubwa ikiwemo Uwanja wa Mpira wa Nzunguni na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na maji
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Dodoma leo, Agosti 31, 2025, Dkt. Samia alisema ifikapo mwaka 2027 ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato utakuwa umekamilika na kuanza kutumika rasmi, hatua itakayowezesha wageni kutoka mataifa mbalimbali, hususan watakaokuja kushuhudia mashindano ya AFCON, kutua moja kwa moja jijini Dodoma.
Vilevile, alibainisha kuwa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Nzunguni jijini Dodoma utakamilika kwa wakati, jambo litakaloongeza hadhi ya jiji hilo kama kitovu cha michezo na makao makuu ya nchi.
Pamoja na miradi ya viwanja, Dkt. Samia alisema serikali yake itaendelea kutatua changamoto ya maji kwa Mkoa wa Dodoma kupitia mradi mkubwa wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria. Alisisitiza kuwa mradi huo utakuwa suluhisho la kudumu kwa wakazi wa jiji hilo.
Kuhusu nishati, amesema mradi wa umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unatarajiwa kukamilika na hivyo kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya wananchi na uwekezaji wa viwanda.
Dkt. Samia pia alitaja kuwa uwepo wa viwanda kupitia mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) utasaidia kuongeza thamani ya mazao na kutoa ajira kwa vijana wa Dodoma na kanda jirani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Balozi Dkt. Bashiru Ali Kakurwa, akizungumza katika mkutano huo, amesema kazi kubwa inayowakabili wanachama na viongozi wa chama ni kwenda nyumba kwa nyumba, shina kwa shina, tawi kwa tawi na kata hadi wilaya kueleza uwezo na ubora wa wagombea wa CCM kuanzia nafasi ya urais, wabunge hadi madiwani.
Ameongeza kuwa kazi nyingine muhimu ni kutetea rekodi ya utendaji wa chama kwa miaka mitano iliyopita pamoja na kufafanua ahadi zilizomo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.
Balozi Dkt. Bashiru pia alisema Halmashauri Kuu ya CCM imegawa nchi katika kanda 11 kwa ajili ya kampeni, ambapo kanda ya Dodoma, Singida na Tabora ni miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao.