Na Meleka Kulwa – Dodoma
Chamwino, Dodoma – Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameanza rasmi kampeni zake mkoani Dodoma leo Agosti 31, 2025 kwa kuzungumza na wananchi wa Chamwino, akitoa shukrani kwa baraka na msaada waliompatia wakati alipokwenda kuchukua fomu ya kugombea urais.
Akihutubia wananchi na viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali, Dkt. Samia amesema alipata baraka za wana Chamwino pamoja na kuchangiwa fedha za fomu, jambo alilolieleza kuwa ni heshima kubwa kwake.
“Baraka huanzia nyumbani, na nyinyi mmenipa baraka kabisa kabisa,” amesema huku akisisitiza kuwa safari ya kampeni ni ndefu na inahitaji maombi na dua kutoka kwa wananchi.
Katika mkutano huo, amesema kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa Chamwino, hasa kutokana na ongezeko la watu.
Aidha, amewahidi wananchi kuwa serikali yake itaongeza ujenzi wa miundombinu ya kijamii, ikiwemo kujenga vituo vya afya kumi na zahanati tano mpya katika Jimbo la Chamwino. Pia, amesema serikali itahakikisha tatizo la maji linatatuliwa kwa kupeleka huduma ya maji karibu na kila mwananchi.
Vilevile, Dkt. Samia amewahakikishia wananchi wa Chamwino ujenzi wa barabara, ambapo kilomita kumi za barabara kwa kiwango cha lami zitajengwa ndani ya mji wa Chamwino. Ameongeza kuwa barabara za changarawe katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Ihumwa – Iyumbu – Dabalo – Segala – Fufu – Shiboli – Mvumi Mission hadi Manzese, zitaboreshwa ili ziweze kupitika wakati wote.
Kwa upande wa kilimo, amesema serikali itaanzisha mashamba makubwa kwa vijana, mfano wa mashamba yaliyopo Chinangali, ili kuwawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha, amesema ombi la kuanzishwa kwa Halmashauri mpya Chamwino limepokelewa, na serikali italiangalia kwa uangalifu kutokana na umuhimu wa eneo hilo.
Amesisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee kinachoweza kusimamia maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanakipigia kura chama hicho pamoja na wagombea wake wa ubunge na udiwani.
“Nawaombeni sana, twendeni tukafanye kampeni kwa bidii, wana Chamwino,” amesema Dkt. Samia.
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia CCM, Deogratius Ndejembi, amesema mvua zinapoanza kunyesha husababisha changamoto kubwa kwa wananchi wa Tarafa ya Itiso, zikiwemo wajawazito kushindwa kuvuka na biashara kukatika.
Amesema serikali imetenga shilingi bilioni 14.5 kwa ujenzi wa daraja la Chilonwa na imefanya maboresho katika elimu na afya wilayani humo.
Ndejembi ameahidi kuwa endapo atachaguliwa ataendelea kuwasilisha maombi ya wananchi kwa Rais, ikiwemo kupandisha Chamwino hadhi ya Halmashauri ya Mji, huku akibainisha kuwa maendeleo yaliyotekelezwa tayari yanaonekana wazi.