NA JOHN BUKUKU- KONDOA
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema wataendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo cha kisasa katika maeneo ya Pahi, wilayani Kondoa.
Dkt. Samia amefafanua kuwa serikali itarekebisha barabara zote ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka.
Aidha, amesema kuwa wananchi wa Kondoa wanapaswa kuwa na matumaini makubwa katika miaka ijayo kwani miradi mingi iliyobaki itakamilishwa ili kuwanufaisha moja kwa moja.
“Kuna ile miradi ya kitaifa ambayo inawanufaisha watu wote, lakini ndani ya Kondoa, ilani ya uchaguzi iliyopita imetuambia vijijini tufanye kwa asilimia 85. Nashukuru wilaya ya Kondoa tumefika asilimia 89. Kwa hiyo, kazi yetu miaka mitano ijayo ni kuhakikisha kila mkazi wa Kondoa anapata maji,” alisema Dkt. Samia.
Amesema kuwa, katika sekta ya afya bado kuna mahitaji makubwa licha ya kazi kubwa kufanyika katika hospitali ya wilaya. Ameahidi kuongeza vituo vya afya na zahanati ili kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.
Kwa upande wa elimu, Dkt. Samia amesema serikali itajenga madarasa mapya kutokana na uhitaji uliopo. Pia, itaongeza shule za sekondari na shule za msingi pamoja na nyumba za walimu.
“Kwenye upande wa afya tutaongeza vituo vinne na zahanati tano. Pia, tutakamilisha vituo vinavyoendelea kujengwa ambavyo bado havijakamilika,” alisema.
Akizungumzia sekta ya miundombinu, Dkt. Samia amesema barabara nyingi ndani ya Kondoa zitajengwa na kukarabatiwa. Ameahidi kujengwa kwa daraja la Bumbuli na daraja la Mto Bubu linalounganisha eneo la Sela na mjini Kondoa.
Amefafanua pia kuwa barabara inayotoka Hospitali ya Wilaya hadi Puma itajengwa kwa kiwango cha lami, sambamba na maboresho ya barabara za vijijini ili zipitike kwa urahisi mwaka mzima.
Dkt. Samia amesema serikali itatekeleza mradi wa skimu ya umwagiliaji katika eneo la Bereko yenye ukubwa wa hekta 150 ili kuwawezesha wakulima kulima mara mbili kwa mwaka.
Vilevile, amesema serikali itaboresha mazingira ya biashara kwa kutenga maeneo ya uwekezaji katika Pahi na kujenga soko kubwa katika kijiji cha Bukulu ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Kondoa.