Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahitibia wananchi wa wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
…………
NA JOHN BUKUKU- KILOSA
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kilosa, Profesa Paramagamba Kabudi, awaeleza wananchi mafanikio yaliyofanywa na mgombea urais kwa kipindi cha miaka mitano.
Kabudi ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye uwanja wa Kilosa mjini, wilayani Kilosa.
Kabudi amesema kuwa sisi tunakushukuru kwa mengi. Mwaka 2020 ulitukabidhi ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kutekeleza.
“Miradi yote uliyoiahidi Mheshimiwa Rais mwaka 2020 katika elimu, afya, maji, miundombinu, mawasiliano na kila kitu umekitekeleza, na hiyo ndiyo iliyonipa ujasiri wa kusema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi yote uliyotuahidi umeitekeleza,” amesema.
Akizungumza kuhusu sekta ya elimu, amesema kuwa alitoa ahadi kuwa kata zote ambazo hazina shule za sekondari zijengewe shule, na sasa kata 3 kati ya kata 25 ndizo zilizokuwa hazina shule ya sekondari.
“Katika kipindi chako hiki, sekta ya elimu peke yake umetuletea jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 26 ambazo zimejenga madarasa mapya 320, shule mpya za msingi 9, shule za sekondari 10, na katika shule hizo mpya za sekondari 10 kata 6 tumejenga shule ya pili. Umeenda zaidi ya ahadi uliyotoa, ndiyo maana nasema hatukudai. Wamejenga pia nyumba za walimu na kukarabati ofisi za walimu. Kulikuwa na high school tatu, lakini katika kipindi chako umetupa high school mpya 6.”
Ameongeza kuwa, kwa upande wa afya umefanya mambo makubwa sana. Sekta ya afya imepata jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 6, na tumejenga vituo vipya vya afya 8. Tulikuwa na vituo 3, umeongeza 8, tumejenga zahanati 20, ICU moja, maabara moja na tumekarabati hospitali ya wilaya ya Kilosa.
Ameongeza kuwa wamepewa ambulance mbili mpya; moja ipo hospitali ya wilaya na nyingine ipo kwenye kituo cha afya.
Amesema kuwa kwa upande wa miundombinu, ujenzi wa daraja la Bereja lenye urefu wa mita 140 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 7, na uwepo wa daraja hilo limewapunguzia gharama ya kwenda Morogoro.
Ameongeza kuwa kwa upande wa barabara, wameanza barabara mpya ya kutoka Mvumi kwenda Ngege kwa gharama ya shilingi milioni 799, na sasa umetuongezea zaidi ya shilingi bilioni 1.
Amefafanua kuwa wamefungua barabara katika maeneo ambayo hayakuwa na barabara, ambapo imewasaidia sana kurahisisha mawasiliano hususan kupeleka wagonjwa. Sasa kutoka mwendo wa dakika 40 ni dakika 10 kufika Kilosa.
Ameongeza kuwa mji wa Kilosa ni mji ambao umekuwa unapambana na mafuriko kwa muda mrefu. Watu wa kata ya Mvumi hawakulala mvua zikinyesha, lakini katika miaka ya uongozi wako tumechimba mifereji na mitaro. Leo hii kata ya Mvumi mafuriko ya mwaka juzi hawakuona hata tone moja la mafuriko, na sasa tunaendelea na kata zingine ikiwa ni pamoja na kuimarisha kingo.
Amefafanua kuwa katika sekta ya maji umetuletea zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.
Ameongeza kuwa sekta ya umeme vijijini, Jimbo la Kilosa lina vijiji 82 na kati ya hivyo ni vijiji 16 tu vilivyokuwa na umeme. Wewe umehakikisha vijiji vilivyobaki vyote leo vina umeme, na sasa kazi yetu ni kupeleka umeme kwenye vitongoji.
Amesema kuwa katika sekta ya kilimo umetoa zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa ajili ya scheme ya umwagiliaji ya Ludewa. Mvua za mwaka jana zilileta changamoto lakini tayari marekebisho yanafanywa, na kwa sasa tuna scheme kubwa ya Mvumi ambayo umeikarabati kwa zaidi ya shilingi milioni 2. Na katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ludewa umeipangia kuongeza scheme nyingine ya umwagiliaji.
“Nimeipitia ilani, ina mambo mazuri ya Kilosa. Moja, Mheshimiwa Rais, nikushukuru kwa uamuzi wa kujenga soko la kisasa hapa Kilosa. Pia tunakushukuru sana kwa kuamua kujenga maghala matano katika ushoroba wa SJR, na tumechonga barabara mbili,” amesema.