Na Mwandishi Wetu, Karatu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Charles Kichere,ijumaa tarehe 29.08.2025 amefanya ziara maalum kwenye jengo la Makumbusho ya Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark pamoja na kupanda mti wa kumbukumbu kwenye Eneo la Makumbusho hayo.
CAG Kichere ambaye aliongozana na mwenyeji wake, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Bw. Abdul-Razaq Badru na menejimenti yake, amejionea na kujifunza urithi wa kitamaduni unaoelezea upekee wa vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro, shughuli za utamaduni, urithi na historia za makabila mbalimbali
Akiwa ndani ya Jengo hilo, CAG Kichere alipata maelezo kutoka kwa Afisa Uhifadhi Mkuu Dr. Agnes Gidna ambaye ni Mtaalam wa Urithi wa Utamaduni NCAA, ambapo alionekana kufurahishwa na namna NCAA ilivyowekeza kwenye Makumbusho hiyo ambayo itatumika kama kivutio cha utalii pamoja na kujifunza kwa wadau mbalimbali.
Hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai unatokana na urithi wa kijiolojia, kiikolojia na kiutamaduni unaojumuisha Mlima Lengai wenye Volkano hai ya kipekee duniani na eneo la Ngorongoro lenye historia ya binadamu wa kale pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo na urithi wa utamaduni wa jamii za wafugaji zilizopo ndani ya Hifadhi.