Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi wa mjini Morogoro wakati alipohutubia mkutano wa Kampeni Leo Agosti 29, 2025 kwenye uwanja wa. Tumbaku mjini humo.
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwapungia mkono wananchi Mara baada ya kuwahutubia wa mjini Morogoro kwenye mkutano wa Kampeni uliofanyika uwanja wa Tumbaku mjini humo.
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapungia wananchi mkono Mara baada ya kumaliza kuhutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Tumbaku Morogoro.
PICHA NA JOHN BUKUKU- MOROGORO
……………..
NA JOHN BUKUKU- MOROGORO
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Mkoa wa Morogoro unaendelea kupata viwanda vipya vikubwa na vidogo, na kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali yake itahakikisha vinaimarishwa ili kurejesha hadhi ya Morogoro kuwa mkoa wa viwanda.
Dkt. Samia ameyasema hayo Agosti 29, 2025, akiwa mkoani Morogoro katika muendelezo wa kampeni za CCM kunadi sera na kuomba kura za wananchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025. Alibainisha kuwa jitihada hizo zitasaidia kuvutia uwekezaji, kuendeleza viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa mkoa huo.
Akieleza vipaumbele vyake, alisema serikali itawekeza zaidi kwenye miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mahenge yenye urefu wa kilomita 67 na barabara ya Kibena–Lupembe–Madeke yenye urefu wa kilomita 105 inayounganisha Njombe na Morogoro. Aidha, kupitia mradi wa kimkakati wa reli ya kisasa (SGR), maendeleo ya viwanda katika eneo la ushoroba wa reli yataimarika zaidi.
Amesema Morogoro pia itafunguliwa kiutalii kwa kujenga miundombinu itakayovutia wageni. Ujenzi wa barabara kutoka kituo cha usafiri kwenda Hifadhi ya Mikumi unatarajiwa kuongeza idadi ya watalii. Vilevile, serikali imepanga kujenga Morogoro Convention Centre, kituo kikubwa cha mikutano kitakachowezesha mkoa huo kupokea wageni wengi kwa shughuli za kikazi, kibiashara na utalii.
Kuhusu sekta ya ardhi, Dkt. Samia alieleza kuwa serikali yake imetoa hati za kimila na zile za serikali ili kumaliza migogoro. Iwapo atachaguliwa, ataendeleza mpango huo kwa kuhakikisha wananchi wanapata hati za kumiliki ardhi ili kuendeleza kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wa kilimo, alisema mkazo utawekwa kwenye ruzuku ya mbolea, upatikanaji wa mbegu bora na uanzishwaji wa vituo vya zana za kilimo ili kuongeza tija. Aidha, maghala matano mapya yataanzishwa katika Wilaya ya Kilosa, yakijengwa kwenye maeneo ya ushoroba wa reli ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.
Soko la kisasa litajengwa mjini Morogoro kwa ajili ya wajasiriamali na wamachinga, huku masoko mengine ya kisasa yakiendelea kujengwa Kilosa na Malinyi. Hatua hizi, amesema, zitachochea biashara, kuongeza kipato na kutoa ajira mpya kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Samia amewataka viongozi wa CCM na wananchi kushirikiana kuhakikisha chama kinapata kura nyingi za ushindi.
Amewaomba wananchi wa Morogoro kumpigia kura yeye kwa nafasi ya Urais, Abdulaziz Abood Mohamed kwa nafasi ya Ubunge wa Morogoro Mjini, pamoja na wagombea wengine wa CCM kwa nafasi za ubunge na udiwani.
Amesisitiza kuwa ushindi wa kishindo utasaidia kuendeleza kasi ya maendeleo na kuufanya Morogoro kuwa kitovu cha viwanda, utalii, biashara na kilimo nchini.