Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 29, 2025,nakimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo ka Morogoro Kusini Mashariki wakati akihutubia mkutano wa kampeni zake Ngerengere katika Wilaya ya Morogoro Vijijini , mkoani Morogoro
…………….
NA JOHN BUKUKU -NGERENGERE
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 29, 2025, amehutubia mkutano wa kampeni zake Ngerengere katika Wilaya ya Morogoro Vijijini , mkoani Morogoro, huku akiwaomba kumpigia kura maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza.
Akihutubia wananchi wa Ngerengere, Dkt. Samia amesema kuwa katika sekta ya afya, miaka iliyopita kulikuwepo vituo vya afya vitano na zahanati 60, lakini sasa vimeongezeka hadi vituo vya afya 11 na zahanati 97.
Aidha, alikiri kupokea ombi la diwani wa eneo hilo la kuanzishwa kwa kituo kikubwa cha afya. Alisema awali Ngerengere walikuwa na changamoto ya chumba cha kuhifadhia maiti na kulazimika kuwapeleka wafiwa Morogoro mjini. Hata hivyo, sasa wamejenga chumba kipya cha kuhifadhia maiti ndani ya Kituo cha Afya cha Ngerengere, hali itakayopunguza gharama kwa wananchi.
Kwa upande wa elimu, alisema serikali imejenga shule za msingi saba na madarasa 120, pamoja na shule mpya za sekondari saba kwenye kata tisa, huku yakiwepo madarasa mapya 95. Hatua hii inalenga kuwawezesha watoto kunufaika na sera ya elimu bila malipo.
Akizungumzia nishati, Dkt. Samia alisema kupitia mradi wa REA vijiji vyote 149 na vitongoji 417 vya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vimepatiwa umeme.
Kuhusu miundombinu ya usafirishaji, alisema ujenzi wa kituo cha SGR ni mkombozi mkubwa kwa Morogoro, kwani kimefungua mkoa kiuchumi. Aidha, Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo zimepanga kujenga ghala kubwa la kuhifadhia mazao katika kituo hicho ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni.
Aliongeza kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Zomozi–Ngerengere yenye urefu wa kilomita 11.6. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 24, na serikali ina mpango wa kukamilisha barabara hiyo kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wa kilimo, alisema serikali imeleta mbolea ya ruzuku na kuwekeza katika kilimo cha kisasa. Pia wameanzisha kituo cha uzalishaji wa zao la tikiti maji na kugawa miche zaidi ya 80,000 kwa wakulima bure. Aidha, maafisa ugani wamepewa pikipiki 68 na vifaa vya kupima udongo ili kuboresha kilimo na kuongeza tija.
Dkt. Samia alisema serikali imejenga maghala matatu mapya, wakati mwaka 2020 hakukuwa na ghala hata moja. Vilevile, imeanzisha mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao ya ufuta, mbaazi na korosho, hatua iliyoleta bei nzuri kwa wakulima.
Aliongeza kuwa zaidi ya kilo milioni nne za mazao zimeshughulikiwa kupitia mfumo huo, na minada mipya miwili imeanzishwa kwa ajili ya wafugaji. Aidha, mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 imetolewa kwa wanufaika 7,015 kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri.
Kuhusu viwanda, alisema kwa sasa Ngerengere ina kiwanda kikubwa kimoja, viwanda vya kati viwili na viwanda vidogo 54 ambavyo vimeongeza ajira kwa vijana wa eneo hilo.
Aidha, alizungumzia sekta ya maji na kusema kuwa, licha ya changamoto zilizopo, serikali imetekeleza miradi 15 ya maji tangu mwaka 2020, na kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 51 hadi 57. Hata hivyo, changamoto bado zipo kutokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti na uchomaji mkaa.
“Tutashirikiana na wananchi kurejesha hali ya mazingira ili kulinda vyanzo vya maji. Katika miaka mitano ijayo, suala la maji litapewa kipaumbele zaidi ili kuongeza upatikanaji wake kwenye maeneo yote ya halmashauri hii,” alisema Dkt. Samia.
Jana Agosti 28, 2025, CCM ilizindua kampeni zake kitaifa kupitia mkutano mkubwa uliofanyika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.