Waziri wa kilimo Mhe. Husseni Mohamed Bashe amekidhi vigezo na kuteuliwa Kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Nzega Mjini, Mkoa wa Tabora.
Mhe. Bashe ambaye ni mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo hilo, sasa anaruhusuwi ya kuanza kunadi sera za Chama Cha Mapinduzi, huku akikabiliwa na mpinzani mmoja kutoka Chama cha ACT wazalendo Bw. Kebelelo Ezra Josiah.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Nzega Mjini Ni. Joyce Emannuel alisema Mhe. Bashe na Bw. Josiah pekee ndio waliokidhi vigezo vya kisheria na hivyo kuteuliwa kuwania nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani utakaofanyika 29 Oktoba mwaka huu.
“Jumla ya wagombea sita kutoka vyama sita vya siasa vilijitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Ubunge kwenye jimbo hili, lakini wengine hawakukidhi vigezo, na baadhi yao wameingia mitini, na hivyo, sifa za uteuzi kubaki kwa Mhe. Bashe na Bw. Josiah Pekee,” alisema Msimamizi wa Uchaguzi.
Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi jimbo la Nzega Mjini, Bwana Omary Mungi, aliwakumbusha wagombea hao kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Bw. Mungi alisisitiza kuheshimu ratiba ya kampeni inavyoainisha muda, terehe na mahala kampeini za chama husika zilipopangwa kufanyika. Aliongeza kuwa hii itaondoa migongano na vurugu kwenye zoezi zima la Uchaguzi mkuu na hivyo kudumisha demokrasia ya vyama vingi.
Awali, wagombea hao walirejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge kwenye Jimbo la Nzega Mjini, na hivyo, kukidhi vigezo vya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha kusaka ridhaa ya wapiga kura kitakacho anza rasmi tarehe 28/08/2025 hadi tarehe 28/10/2025.