Na Silivia Amandius.
BUKOBA
Almsoud Dauda Kalumuna ameibuka tena katika ulingo wa siasa baada ya kukabidhiwa rasmi fomu ya kugombea ubunge kupitia chama cha ACT Wazalendo katika Jimbo la Bukoba Mjini. Hatua hiyo inamfanya kuwa mgombea halali wa chama hicho katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Bukoba Mjini, Melkion Komba, amethibitisha kuwa Kalumuna amekidhi vigezo vyote vya kisheria na tayari amekabidhiwa barua rasmi ya kuthibitisha kugombea. Komba alisisitiza kuwa mgombea huyo anatakiwa kujaza na kurejesha fomu hiyo kabla ya tarehe ya mwisho ya Agosti 27, 2025, kama inavyoelekezwa kwenye ratiba rasmi ya uchaguzi.
Akizungumza baada ya kupokea fomu yake, Kalumuna alisema kuwa ana dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Bukoba Mjini. Alitoa wito kwa wakazi wa jimbo hilo kumkaribisha kwa ushirikiano, akiahidi kushirikiana nao katika kujenga uchumi na huduma bora za kijamii.
Kalumuna aliwahi kuwania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo katika kura za maoni alipata kura 640 na kushika nafasi ya tatu. Alitanguliwa na Eng. Johnston Mtasingwa ambaye sasa ni mgombea rasmi wa CCM kwa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Bukoba Mjini