NA SOPHIA KINGIMALI
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Geofrey Timoth, ameishukuru Kamati Kuu ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kupeperusha bendera ya chama katika jimbo hilo.
Akizungumza leo, Agosti 26, 2025, mara baada ya kuchukua fomu kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Timoth aliwataka wananchi wa Kawe kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni unaotarajiwa kufanyika Agosti 28, 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Pekars, Kawe.
Amesema yapo mambo mengi ambayo wamepanga kuyatekeleza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Kawe, na kwamba atayafafanua wakati wa kampeni rasmi zitakapoanza.
“Kampeni bado hazijaanza, tutawaeleza wananchi mambo tunayotarajia kuyafanya. Kwa leo nawashukuru wajumbe na viongozi wakuu wa chama kwa kuniteua kupeperusha bendera ya chama katika Jimbo la Kawe,” alisema Timoth.
Ameongeza kuwa, “Tarehe 28 tunalo jambo kubwa. Wanakawe tujitokeze kwa wingi kwenye uzinduzi wa kampeni ili tumuunge mkono Mama (Dk. Samia), lakini pia tusikilize yale mambo ambayo chama kimejipanga kuyatekeleza.”