Dar es Salaam, 25 Agosti 2025
Shirika la Posta Tanzania limefungua ukurasa mpya wa ubunifu wa huduma zake kwa kushirikiana na Klabu ya Simba SC, kupitia udhamini wa tukio la Simba Day litakalofanyika tarehe 10 Septemba 2025.
Akizungumza katika hafla ya kutangaza tarehe rasmi ya Simba Day iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika hilo, Bw. Ferdinand Kabyemela, alisema ushirikiano huo ni zaidi ya udhamini, kwani unalenga kuongeza ukaribu wa huduma za Posta na jamii, hususan vijana.
Kupitia makubaliano hayo, Shirika la Posta litakuwa msambazaji rasmi wa bidhaa za Simba SC kama jezi na tiketi, zikisambazwa kupitia mtandao mpana wa ofisi za posta nchini kote. Hatua hii itarahisisha mashabiki wa Simba kupata bidhaa halisi na salama karibu na walipo, huku ikifungua milango ya matumizi ya huduma nyingine za Posta.
“Tunataka huduma za kisasa za Posta ziwe sehemu ya maisha ya vijana. Kupitia Simba Day, tunafikisha huduma zetu za usafirishaji wa mizigo, EMS, huduma za kifedha na biashara mtandao kwa urahisi zaidi,” alisema Kabyemela.
Aidha, nembo za Posta zitakuwa zikionekana kwenye jezi, mabango, matangazo ya televisheni na mitandao ya kijamii ya Simba SC yenye mamilioni ya wafuasi, jambo litakaloongeza hadhi na umaarufu wa Shirika katika soko la kidigitali.
Wachambuzi wa sekta ya michezo na biashara wanaona hatua hii kama mfano bora wa mashirikiano kati ya huduma za jadi na ulimwengu wa michezo, unaosaidia kuunganisha urithi wa posta na kizazi kipya cha kidigitali.
Kwa mashabiki wa Simba na wananchi kwa ujumla, Simba Day ya mwaka huu haitakuwa tu sherehe ya mpira wa miguu, bali pia fursa ya kuona jinsi taasisi kongwe kama Posta inavyojibadilisha ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Jamie.