Namtumbo
WAKULIMA wa zao la Tumbaku katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wameonywa kuacha tabia ya kiuni kutia maji na kuchanganya uchafu kwenye Tumbaku kwani kufanya hivyo kunaharibu na kupunguza ubora wa zao hilo.
Hayo yamesemwa jana na Meneja Shughuli wa Kampuni ya Premium Active Tanzania Makaka Shaban,wakati akizungumza na wakulima wa Tumbaku wanaohudumiwa na Chama cha msingi cha ushirika Nambecha Amcos kata ya Mgombasi Wilayani humo.
Alisema, baadhi ya wakulima wanafanya vitendo vya udanganyifu kuchanganya tumbaku mzuri na mbaya na wengine kuweka maji na matofali kwa lengo la kuongeza uzito jambo ambalo Kampuni hiyo haitakuwa tayari kufanya biashara na wakulima hao.
Makaka amesisitiza kuwa,zao hilo kama yalivyo mazao mengine ya kibiashara ni zao la kimkakati linalohitaji uangalizi mkubwa na matumizi sahihi ya mbolea ili kupata tumbaku yenye ubora na kukubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.
Makaka alieleza kuwa,tumbaku bora inavutia wanunuzi,hivyo kuwaongezea kipato wakulima na hatimaye kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kwenye familia na kuchangia pato la Taifa.
Alisema,sehemu kubwa ya uchumi wao wanategemea kilimo cha zao la Tumbaku,hivyo Kampuni ya Premium Active Tanzania itahakikisha inaweka mazingira mazuri na rafiki kwa wakulima ikiwemo kuongeza motisha ili waweze kuendelea kuzalisha bila vikwazo.
Makaka,amewakumbusha wakulima kuzingatia taratibu na sheria za uzalishaji wa zao hilo kama wanavyoelekezwa na maafisa ugani ili kuepuka hasara kwao na kampuni na kushuka kwa uchumi wao na Serikali kwa ujumla.
Alisema,wasipozingatia taratibu na kanuni za kilimo cha Tumbaku watajisababishia hasara kwani Tumbaku yao itakataliwa kwenye minada na Halmashauri kukosa mapato na uchumi wa Taifa kushuka.
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Nambecha Amcos Rajabu Saidun,ameishukuru Kampuni ya Premium kwa kununua Tumbaku inayozalishwa na wakulima wa kijiji hicho kwani tangu ilipoanza wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa soko na bei.
Alisema,awali kabla ya kuingia kwa Kampuni ya Premium hali ya maisha ya wakulima ilikuwa mbaya kwani baadhi yao waliacha kulima zao hilo kwa kukosa soko la uhakika na kupelekea maisha yao kuwa magumu.
Alisema,changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya wakulima kulisha tumbaku yenye ubora mdogo na wengine kuchanganya na uchafu hali iliyosababisha wakulima hao kupata hasara kubwa.