Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
24/8/2025 Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila wameungana katika matembezi ya kilomita tano ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Matembezi hayo yaliyofanyika jana yalianzia kwenye Viwanja vya Green Park na kuishia katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam yaliambatana na zoezi la upimaji wa afya ya moyo kwa wanamichezo walioshiriki katika matembezi hayo.
Akizungumza mara baada ya kushiriki matembezi hayo Mhe. Chalamila aliipongeza JKCI kwa kutoa huduma bora za matibabu ya moyo na kutoa wito kwa jamii kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Niipongeze JKCI kwa huduma bora zinazovuka mipaka ya nchi. Miaka 10 ya huduma imeleta mageuzi makubwa katika matibabu ya moyo nchini. Ni jukumu lenu kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kuwa bora”.
“Niwaombe wakazi wa Dar es Salaam tukutane kila Jumamosi kufanya mazoezi kwa afya zetu. Ni wajibu wetu kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza”, alisema Mhe. Chalamila.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema katika maadhimisho hayo jumla ya wanamichezo 5,000 wamefanyiwa vipimo vya moyo ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa huduma mpya ya upimaji wa afya ya moyo kwa wanamichezo.
“Tumefanya vipimo kwa wachezaji wa Simba, Yanga na Azam, pia wanafunzi na wanamichezo mbalimbali, ili waweze kujua hali ya afya za mioyo yao kabla ya kuanza michezo”, alisema Dkt. Angela.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilianzishwa tarehe 5 Septemba 2015 kwa Sheria ya mwaka 2015 kupitia tangazo la serikali namba 454. JKCI inatoa huduma za ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi hasa zile zinazopakana mipaka na Tanzania ambazo ni Kenya, Malawi, Visiwa vya Comoro, Zambia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zimbabwe, Sudani na Somalia.