Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemteua rasmi Dkt. Asharose Migiro kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho tawala. Uteuzi huo umetangazwa leo kufuatia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Migiro anachukua nafasi hiyo kufuatia mabadiliko yaliyofanyika ndani ya uongozi wa chama, ambapo uteuzi wake umetajwa kuwa sehemu ya juhudi za chama kuimarisha utendaji wake wa kisiasa na kiuongozi katika kipindi hiki cha mageuzi na maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu.
Akiwa ni Mwanadiplomasia mashuhuri na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa, Dkt. Migiro aliwahi kuhudumu kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.