* Serikali yasaini mkataba wa nyongeza ya hisa kutoka asilimia 16 hadi 20 na Kampuni ya Nyanzaga
* Mwekezaji arejesha Leseni Serikalini, Waziri Mavunde aagiza kupewa wachimbaji wadogo
*Mradi kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 1
* Ni mgodi mkubwa wa dhahabu kuanzishwa tangu 2009
▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira wezeshi ya Uwekezaji
Sengerema, Mwanza.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga, unaotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Perseus Mining Limited kupitia Kampuni ya Nyanzaga Mining Company Ltd, utakuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi katika kipindi chote cha utekelezaji wake.
Amesema hayo leo Agosti 20, 2024 katika Kijiji cha Sotta Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya Nyongeza Kati ya Serikali na Kampuni ya Nyanzaga Mining Company Limited kwa Ajili ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Dhahabu Kupitia Kampuni ya Ubia ya Sotta Mining Corporation Limited.
Katika Hafla hiyo, Serikali imesaini mkataba wa nyongeza na Kampuni ya Nyanzaga Mining Limited kutoka asilimia 16 hadi 20 za umiliki wa hisa za Kampuni ya Ubia ya Sotta.
Akizungumza katika Hafla hiyo, Waziri Mavunde amebainisha kuwa zaidi ya shilingi trilioni 1 zinatarajiwa kuwekezwa katika utekelezaji wa mradi huo, hatua ambayo itasaidia kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa Watanzania hususan wananchi wa Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza na taifa kwa ujumla
Ameeleza manufaa ya Mradi huo kuwa ni pamoja na Ajira kwa Watanzania kwani Mradi utatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya wananchi, na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira; Ushiriki wa Watanzania ambapo Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kupitia utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazohitajika kwenye mradi.
Mafanikio mengine ni Mapato ya Serikali kupitia kodi, tozo na gawio la hisa za Serikali (20% free carried interest), ambapo mradi utaiingizia Serikali mapato makubwa ambayo yataelekezwa kwenye miradi ya maendeleo; Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambapo Kampuni hiyo italazimika kushirikiana na jamii katika kuboresha huduma za kijamii kama shule, afya, maji na miundombinu pamoja na kusaidia miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha wananchi na taifa kwa ujumla wananufaika ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Kampuni ya Sotta Mining imerudisha leseni yake Serikalini, na Wizara itahakikisha leseni hizo zinagawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Sengerema huku akiitaka Kampuni ya Sotta kuendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo, na kuagiza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupeleka mtambo maalum wa kuchoronga (drilling rig) ili kusaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija.
Waziri Mavunde ameihakikishia Kampuni ya Perseus kuwa haitajutia uamuzi wake wa kuwekeza Tanzania, kwani taifa lina sera bora, mazingira rafiki ya uwekezaji, na dhamira ya kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus Bi. Lee-Anne de Bruin ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo hayo na hatimaye kusainiwa mkataba huo wa nyongeza kati ya Serikali na Kampuni yetu ambapo utaruhusu shughuli za uzalishaji kuanza pindi shughuli za ujenzi zitakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2027.
“Mradi huu utaleta manufaa makubwa kwa taifa hili mara mbaada ya kuanza uzalishaji. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyosaidia kurahisisha mchakato wa uwekezaji huu mkubwa.” Amesema Bi. Lee-Anne.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameeleza kuwa kiasi cha fedha cha dola za Marekani milioni 500 zitakazotumika kujenga mradi huo, zitasaidia kubadilisha Mkoa wa Mwanza, na kwamba kuanzishwa kwa mradi huo utasaidia zaidi kuongeza mapato ya Serikali katika Mkoa huo.
Awali akizungumza, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ameeleza kuwa, Mgodi huo utaletea taifa maendeleo endelevu, ni moja ya miradi mikubwa zaidi ya madini Tanzania na utaleta faida kubwa kwa taifa na kwamba utaingizia Serikali shilingi bilioni 400 lakini pia mapato kupitia Kodi, gawio na vitu vingine, lakini pia utaleta ajira,
“mradi huu utaimarisha uchumi wetu, katika kipindi cha mnyukano wa uchumi duniani, kilichotusaidia ni madini, ni bidhaa inayotuletea fedha nyingi sana za kigeni na kusaidia kuimarisha uchumi wetu” amesisitiza Mchechu.