Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya akizungumza na wananchi wa Kata ya Kimbiji leo 20 Agosti, 2025 wakati akitoa elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia, umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni wakitoa elimu ya matumizi ya Nishati safi ya Kupikia kwa wakazi wa Kata ya Kimbiji.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni, limeendelea kutekeleza wa wajibu wa kijamii kwa kuwajengea wananchi uelewa kwa kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia, umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
Zoezi hilo limefanyika katika Kata ya Kimbiji, Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, likiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika, endelevu, salama na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza leo 20 Agosti 2025 wakati wa kutoa elimu hiyo kwa wakazi wa Mtaa wa Kizito Huonjwa, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhamasika kutumia nishati safi ya kupikia ya majiko yanayotumia Nishati ya umeme (majiko ya kisasa) yanayotumia teknolojia rafiki kwa mazingira.
Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi si tu yanaboresha afya za watumiaji kwa kupunguza moshi unaotokana na kuni na mkaa, bali pia yanasaidia kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti ovyo.
“Ni wakati sasa kwa wananchi wetu kutambua kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana faida nyingi, ikiwemo gharama nafuu, kuokoa muda wa kupika, na zaidi ya yote kulinda mazingira yetu. TANESCO inaendelea kuwaelimisha wananchi ili kuhakikisha wanatumia majiko haya majumbani,” amesema Bi. Mahwaya.
Aidha, Bi. Mahwaya amesisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme kwani ni mali ya umma inayochochea maendeleo, huku akionya dhidi ya vitendo vya uharibifu wa makusudi au wizi wa miundombinu ya umeme kutokana athari zake ni kubwa kwa uchumi na usalama wa jamii.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Bw. Henry Martin, ameeleza kuwa TANESCO inaendelea na juhudi za kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote wa maeneo ya Kimbiji na maeneo jirani.
Amesema kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mikakati ya shirika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora ya umeme inayowezesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Shirika linaendelea na jitihada za kuhakikisha mitaa yote inafikiwa na huduma ya umeme kwa wakati. Tumeshuhudia faida katika maeneo yaliyopata umeme, ambapo shughuli za kiuchumi kama vile biashara, usindikaji wa mazao na utoaji wa huduma za kijamii kama afya na elimu zimeimarika kwa kiwango kikubwa,” amesema Bw. Martin.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Kizito Huonjwa, Bw. Juma Kizenga, amelipongeza Shirika la TANESCO Mkoa wa Kigamboni kwa namna linavyoshirikiana na wananchi na serikali za mitaa katika kuimarisha huduma ya umeme.
Amesema kuwa zaidi ya asilimia 98 ya kaya katika mtaa huo zimepata huduma ya umeme, jambo ambalo limesaidia kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza kipato na kukuza shughuli za kiuchumi.
“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa TANESCO kwa kutufikia na kutupa elimu hii muhimu. Wananchi wetu sasa wameanza kuelewa umuhimu wa kutumia nishati safi na pia wajibu wao katika kulinda miundombinu ya umeme, ni hatua kubwa kuelekea maendeleo endelevu ya jamii yetu,” amesema Bw. Kizenga.
Kupitia mkutano huo wa elimu kwa umma, wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kutoka kwa maafisa wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo huduma ya umeme, utaratibu wa kuunganishiwa umeme mpya, malipo ya bili, pamoja na namna ya kutoa taarifa pindi kunapotokea hitilafu au uharibifu wa miundombinu ya umeme katika maeneo yao.
TANESCO imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwahudumia Watanzania kwa weledi na uwazi, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya shirika hilo na wananchi kama nguzo muhimu ya kufanikisha upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu ya nishati ya umeme nchini.