Na WAF, Mbeya
Timu ya Usimamizi Shirikishi ikiongozwa na Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastiano Millanzi limeendesha elimu ya matumizi sahihi ya miwani ili kuwaepusha watu kujinunulia miwani kiholela.
Elimu hiyo imetolewa Agosti 18, 2025 katika Soko la Kabwe lililopo jijini Mbeya ambapo imebainika kuwepo kwa baadhi ya wafanyabishara ambao hawana taaluma ya Optometria lakini wanajihusisha na uuzaji wa miwani bila kuwapima na kuiuza pamoja na bidhaa nyingine mbalimbali za urembo kinyume na miongozo iliyopo.
Akitoa elimu wakati wa zoezi hilo Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi amesema miwani ni miongoni mwa tiba, hivyo kuziuza kiholela zinaweza kuleta athari kwa mtumiaji, ni vema anayetaka kujihusisha na biashara ya miwani azingatie sheria Optometria sura namba 23 ikiwemo kusajiliwa katika Baraza hilo.
“Kutokujua sheria sio sababu ya kuvunja sheria na ni bahati kuwa ninyi mlikuwa bado hamjapata elimu hii, hivyo kwa sasa tunawapa elimu pamoja na kuwataka kusitisha hadi pale mtakapokamilisha taratibu stahiki za usajili kuanzia ngazi ya Mganga Mkuu wa Jiji, amesisitiza Bw. Millanzi.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao wamekiri kufanya biashara hiyo bila kujua kuwa wanakiuka taratibu, hivyo wakaahidi kuzingatia maagizo yaliyotolewa kwao ya kuanza taraibu za usajili.
Bw. Millanzi ametumia wasaa huo kuziagiza mamlaka za usimamizi ngazi ya halmashauri na mkoa kuwa na muendelezo wa usimamizi shirikishi wa mara kwa mara na kutoa elimu endelevu kwa wananchi.
Timu ya usimamizi kutoka Wizara ya Afya chini ya Baraza la Optometria inashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, ngazi ya mkoa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika kazi hiyo.