Na Sixmund Begashe, Rukwa.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imewakabidhi zaidi ya Mizinga 20O ya nyuki kwa Machifu wa Mkoa wa Rukwa ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufungaji Nyuki kwa Tanzania iliyo Bora ujulikanao kama ‘Achia Shoka Kamata Mzinga’.
Akikabidhi Mizinga hiyo kwa machifu hao wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani humo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, amesema Mpango huo unalenga kuongeza uzalishaji wa asali kutoka tani 33,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 kwa mwaka ifikapo Juni 2035.
CP. Wakulyamba amesema ugawaji wa mizinga hiyo unaunga mkono juhudi za Mhifadhi namba moja nchini Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwainua wanachi kiuchumi kupitia Uhifadhi wa Maliasili hususan Misitu na Nyuki.
“Pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinaendelea kuhifadhiwa Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutangaza na kuvutia wawekezaji kwenye sekta zetu za misitu, ufugaji nyuki, Malikale, wanyamapori na utalii, tunampongeza sana,” amesema CP. Wakulyamba
Aidha, amewaasa Machifu hao na wananchi wote kushirikiana vyema na wataalam wa Wizara hiyo katika kujifunza zaidi namna nzuri ya kufuga nyuki kwa kutumia zana za kisasa pamoja na Uhifadhi endelevu wa rasilimali hiyo, huku akiitaka TFS kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi pamoja na kuendeleza shughuli za utalii katika maeneo hayo.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Msalika Makungu, amebainisha kuwa takwimu zinaonesha, Mkoa una mizinga ya kisasa 5,710, mizinga ya Kienyeji 2,251 na wafugaji 3,736, hivyo jitihada zinazofanywa na Wizara zinakwenda kuimarisha shughuli za ufugaji nyuki Rukwa.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Daniel Pancras amesema sekta ya ufugaji nyuki kwa sasa inachangia ajira takribani milioni 2 ikihusisha wazalishaji wa asali, wachakataji na wafanyabiashara ya asali na vifaa vya kufugia nyuki hivyo jitihada zaidi zinafanyika ili kuongeza fursa zaidi ya zilizopo.