* Azitaka Wizara na Taasisi kutenga Bajeti kusimamia utekelezaji wa Mpango huo
* Awataka Wanawake kupambana katika maeneo waliyopo
* Awashukuru wadau wa maendeleo uandaaji wa Mpango huo
Na WMJJWM- Dar Es Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Mashaka Biteko amezindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Mpango huo Agosti 19, 2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani (TPTC) kilichopo Kunduchi mkoani Dar Es Salaam, Dkt. Biteko amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanatenga Bajeti ya utekelezaji wa Mpango huo ili kutimiza malengo yake.
“Naomba nitoe rai kwa Wizara zote zenye dhamana ya agenda hii; Tanzania Bara na Zanzibar; mkasimamie na kutekeleza mpango huu kama ilivyokusudiwa ili kufikia malengo stahiki” amesema Dkt. Biteko
Aidha Dkt. Biteko amesema katika utekelezaji wa Mpango huo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakiwa Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango huo kwa kushirikiana na wadau waliopo.
“Niwaombe kuhakikisha kuwa mnatoa elimu na kuhamasisha, ushiriki wa wanawake na wanaume katika hatua zote za kuzuia, kutatua migogoro na ujenzi wa amani, ulinzi na usalama.” amesisitiza Dkt. Biteko
Akitoa salamu za Wizara Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika kuandaa Mpango huo, uainishaji wa maeneo mahsusi ya vipaumbele vya Mpango umezingatia maudhui ya Azimio Na. 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa Mpango huo unabainisha maeneo manne (4) ya kipaumbele na kuwasilisha masuala ya msisitizo katika utekelezaji ikiwemo eneo la kuzuia linalosisitiza umuhimu wa kujumuisha mitazamo ya kijinsia katika mikakati ya kuzuia migogoro na mbinu za tahadhari za mapema, eneo la ushiriki linalosisitiza haja ya ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi katika ngazi zote katika michakato ya amani, utatuzi wa migogoro na kujenga amani.
Akiyataja maeneo mengine kuwa ni eneo la ulinzi linalotoa wito wa kuimarishwa kwa hatua za kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia wakati na baada ya migogoro na eneo la Msaada na Urejeshaji wa Hali linalohimiza utekelezaji wa mbinu au jitihada zinazozingatia usawa wa kijinsia katika juhudi za usaidizi na uokoaji na wakati wa urejeshaji wa hali ya ustawi na utulivu baada ya migogoro.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Stergomena Tax amesema Tanzania imetambua kuwa ili kuimarisha amani Wanawake lazima washirikishwe katika Ajenda hii hivyo uwepo wa Mpango huo utaweka mikakati mahususi ya kushirikisha wanawake katika amani na usalama na kuimarisha juhudi za Kitaifa katika kuzuia migogoro kukuza amani jumuishi na kulinda Haki za Wanawake na wasichana.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe amesema Ajenda Wanawake Amani na Usalama ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na Watanzania wote hivyo katika kutekeleza Ajenda hii Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati na mipango mbalimbali katika kuhakikisha Wanawake wanashirikishwa katika masuala ya amani na usalama na kukuza Usawa wa Kijinsia na Ustawi wa Wanawake.
Naye Mkurugenzi wa Kanda wa UN Women Anna Mutabati amesema katika utekelezaji wa Mpango huo Tanzania haianzi mwanzo bali inaendeleza mipango na mikakati iliyopo inayotekelezwa kuhusu masuala ya Wanawake Amani na Usalama chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo utaleta mabadiliko zaidi katika nyanja mbalimbali.