Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu na kuepuka kutumia lugha zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Wito huo ameutoa leo, Agosti 18, 2025, wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa vyama vya siasa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa wa namna ya kutekeleza sheria husika, hivyo amewataka washiriki kusikiliza kwa makini na kuelewa ili wawe mabalozi wazuri wa elimu hiyo kwa wengine.
“Nipende kuwakumbusha ndugu zangu, vyama vya siasa, kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi. Amani ya Taifa ipewe kipaumbele. Nchi ikingia kwenye machafuko hatutakuwa na siasa wala maendeleo, hivyo tuwe mabalozi wa amani,” amesema Jaji Mutungi.
Aidha, amewataka viongozi hao kurithisha amani iliyoasisiwa na viongozi wa Taifa kwa vizazi vijavyo na kuhakikisha wagombea wanakuja na sera nzuri zitakazowavutia wananchi, badala ya kutumia lugha za matusi dhidi ya vyama vingine wakati wa kampeni.
Vilevile, Jaji Mutungi amesisitiza umuhimu wa kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazosambazwa mitandaoni katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Viongozi tunatakiwa kuwa makini sana. Unaweza ukaamka asubuhi ukaona taarifa za uvumi zikidai hakuna uchaguzi. Tuupuuze uvumi huo. Uchaguzi upo na utakuwa wa amani na haki,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, amewataka viongozi na watendaji wa vyama kuzingatia masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuepusha dosari na kasoro katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Amempongeza pia Msajili wa Vyama vya Siasa kwa hatua ya kuwaleta pamoja viongozi na watendaji wa vyama kwa ajili ya elimu hiyo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha demokrasia nchini.
“Tunakupongeza sana Msajili na ofisi yako kwa kazi nzuri ya ulezi wa vyama vya siasa. Umeona umuhimu wa kutukutanisha ili kupitia Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Jambo hili ni jema kwa sababu linapunguza kasoro katika uchaguzi wetu,” amesema Khatibu.
Ameeleza kuwa awali baadhi ya vyama na wagombea walikuwa na uelewa mdogo kuhusu uwasilishaji wa taarifa za gharama za uchaguzi, hali iliyosababisha kasoro ikiwemo kutumia risiti za kughushi kwa kudhani wangerejeshewa fedha baada ya uchaguzi.
> “Sheria hii ilipokuja mwaka 2010 watu wengi hawakuwa na uelewa. Wengine walijaza gharama za uchaguzi hewa wakidhani wangerejeshewa fedha. Hivyo basi, leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha,” amefafanua.
Khatibu amehitimisha kwa kuwataka viongozi na watendaji wa vyama kuchukulia kwa umakini mkubwa mafunzo hayo ili kuhakikisha zoezi la kampeni na uchaguzi kwa ujumla linaendeshwa kwa uwazi, uadilifu na bila migogoro.