Kigoma
Wananchi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wameanza kunufaika na mradi wa TACTIC unaotekelezwa chini ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Akielezea mradi huo unavyotekelezwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji , Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Bw. Kisena Mabuba amesema kuwa mradi huo umejikita katika uboreshaji wa miundombinu ambapo kwa Manispaa hiyo kazi zinazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji, ujenzi wa daraja, masoko na barabara.
Aidha, ameongeza kuwa miundombinu hiyo inayojengwa inalenga kukuza uchumi wa wananchi na kuondoa kero za usafiri na usafirishaji huku akibainisha kuwa kipindi cha masika wananchi walikua wanapata shida kwani maji yaliingia katika makazi yao lakini kupitia mradi wa TACTIC tayari mitaro imejengwa na maji yanaelekezwa moja kwa moja ziwani.
“Kupitia mradi huu, tutapata barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 9.5 ambazo zitaunganisha Kata sita za Manispaa yetu, uwepo wa taa za barabarani pia utapendezesha Mji wetu, “alisema
Kwa upande wake Mhandisi Julius Samwel ambaye ni mratibu wa mradi wa TACTIC ngazi ya Manispaa amesema kuwa miradi yote imeanza na utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali.
Wakiongea kuhusu miradi hiyo wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wameonesha furaha yao juu ya utatuzi wa kero ya muda mrefu.
Bi. Mariam Athumani ambaye ni Mkazi wa Kigoma Ujiji amesema kuwa kabla ya ujenzi wa mifereji ,maji yaliingia katika makazi na kusababisha kero na uharibifu wa mali lakini kwa sasa yameelekezwa moja kwa moja ziwani.
Akiongea kuhusu ujenzi wa Soko la Mwanga Bw. Hussein Hamis ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Kigoma amesema kuwa kukamilika kwa soko hilo kutachochea uchumi wa Mkoa kwani watapata wageni mbalimbali kutoka nchi za jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ambao watafika kufanya biashara.
Kuhusu ujenzi wa Soko la samaki Katonga, wafanyabiashara wameipongeza Serikali kuleta mradi huo utakaowawezesha kufanya biashara kwa njia za kisasa na kukuza uchumi .