Afisa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Bw. Goodluck Assenga akitoa mafunzo kwa wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika mkoa huo yaliyofanyika leo Agosti 15, 2025 jijini Dar es Salaam.
Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Mbagala Verdiana Ndamgoba akitoa elimu ya matumizi ya majiko ya nishati safi ya kupikia kwa wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika mkoa huo.
Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Yombo Angela Kalambo akitoa elimu kwa wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika mkoa huo.
Wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa katika mafunzo
……
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limewajengea uwezo wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika mkoa huo kwa kuwapa elimu kuhusu matumizi ya majiko ya nishati safi ya kupikia, usalama wa wafanyakazi, utunzaji wa miundombinu ya shirika, pamoja na mbinu za kudhibiti wizi wa umeme, ikiwa na lengo la kuwafanya kuwa mabalozi wa shirika katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Agosti 15, 2025, katika Ofisi za TANESCO Mkoa wa Temeke, Afisa Huduma kwa Wateja wa Mkoa huo, Bw. Goodluck Assenga, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwaandaa wanafunzi hao kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kutoa elimu sahihi kuhusu huduma za TANESCO.
Kwa upande wao, wanafunzi waliohudhuria mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopata, huku wakisema kuwa elimu hiyo imewapa uelewa mpana na motisha ya kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii juu ya matumizi bora ya nishati na umuhimu wa kulinda miundombinu ya shirika.
“Kabla ya mafunzo haya, sikuwa nafahamu ni kwa kiwango gani wizi wa umeme unaathiri maendeleo ya shirika na taifa. Sasa najua na nipo tayari kuwa sehemu ya kutoa elimu na kusaidia kuzuia tatizo hili katika jamii,” amesema Rhobina Nyamseti, Mwanafunzi kutoka Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA).
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TANESCO Mkoa wa Temeke katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaopitia mafunzo ya vitendo wanapata uelewa wa kina kuhusu majukumu ya shirika hilo na mchango wao kama vijana katika kusaidia maendeleo ya sekta ya nishati nchini.