Mwamvua Mwinyi, Pwani
Agosti 13, 2025
Mkoa wa Pwani unakadiriwa kuwa na jumla ya wagonjwa wa Siko Seli 6,145, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kupitia mahudhurio ya kliniki kati ya Januari hadi Desemba 2024, huku Wilaya ya Mkuranga ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa.
Tawimu hiyo imebainika, agost 12,2025 wakati wa semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa Siko Seli, iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikisha madaktari bingwa na wataalamu wa magonjwa ya damu.
Dkt. Pius Muzzazzi, Daktari Bingwa wa Watoto na Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbii alieleza licha ya Dar es Salaam kuongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Siko Seli, lakini kati ya wagonjwa wanaopata matibabu katika vituo vya afya vya mkoa huo, asilimia 10 hadi 15 wanatoka Mkoa wa Pwani.
“Kwa Mkoa wa Pwani, kati ya wagonjwa walioripoti kliniki kati ya Januari hadi Desemba 2024 ni 6,145, ambapo Wilaya ya Mkuranga inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,444. Wilaya nyingine ni Kibaha Mjini (1,290), Bagamoyo (1,078), Rufiji (582), Kibiti (541), Kisarawe (510), Chalinze (340), Kibaha Vijijini (305) na Mafia (155),”
Aidha, alihimiza wanandoa, wazazi na jamii kwa ujumla kuchukua hatua ya kupima ugonjwa wa Siko Seli mapema, sawa na jinsi watu wanavyopima magonjwa mengine, ili kuwezesha kupata tiba kwa wakati iwapo ugonjwa utagundulika.
“Watoto wengi hupoteza maisha wakiwa na umri chini ya miaka mitano kwa sababu wazazi hushindwa kubaini mapema kama watoto wao wana ugonjwa wa Siko Seli,” aliongeza Muzzazzi.
Nae Mratibu wa Huduma za Siko Seli kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asteria Mpoto, alieleza semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi wa dini, walimu, waandishi wa habari na makundi mengine ya jamii ili wawe mabalozi wa kutoa elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo, dalili zake na namna ya kukabiliana nao.
Dkt. Asteria alisema ugonjwa huo sio laana bali ni wa kurithi unaosababishwa na vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili na unaweza kudhibitiwa iwapo utagunduliwa mapema na kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu ugonjwa huo, Dkt. Jamila Makame, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Amana, alisisitiza umuhimu wa kupima kabla ya ndoa ili kupunguza hatari ya kupata watoto wenye ugonjwa huo.
Alitaja dalili kuu za Siko Seli kuwa ni upungufu wa damu, maumivu makali ya mwili, kuvimba mikono na miguu, kubanwa kwa kifua, na kuchelewa kukua kwa watoto.
Mkazi wa Kibaha Mjini, Sheikh Mohammed Abdallah Lukemo wa Kata ya Pichandege, alisema wananchi wengi hawana uelewa kuhusu ugonjwa huo na hawajitokezi kupima kama wanavyofanya kwa magonjwa mengine.
“Baada ya kupata elimu hii, nimeamua kupima na nimegundulika sina ugonjwa huo, kwa sasa tunajipanga kuendelea kusambaza elimu hii kwa waumini wetu na jamii ili kupunguza mzigo wa ugonjwa huu,” alielezea Lukemo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mikoa inayoongoza kwa idadi ya wagonjwa wa Siko Seli nchini ni Dar es Salaam, ikifuatiwa na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma.