Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimekumbushwa kuwa ukombozi wa kiuchumi ni safari ndefu na ili kuifikia nchi hizo zinahitaji mtangamano wenye nguvu na usioyumbishwa katika utekelezaji wa malengo waliyojiwekea.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Prof. Amon Murwira kabla ya kukabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Mhe. Rasata Rafaravavitafika jijini Antananarivo Agosti 12, 2025.
Katika Kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na moja ya agenda inayojadiliwa ni maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17, 2025.
Prof. Murwira amesema safari yoyote haikosi changamoto na kutumia jukwaa hilo kuwatahadharisha washiriki wa Mkutano huo kuwa, changamoto zisiwe sababu za kutofikiwa kwa malengo mazuri yaliyoanzisha SADC.
Alisema SADC ilianzishwa kwa lengo la mtangamano wa kikanda, nchi wanachama zinatakiwa zikumbuke hili wakati wote na kukumbuka dhamira njema ya waasisi wa Jumuiya hiyo kama vile, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Robert Mugabe na Hayati Keneth Kaunda.
Amehitimisha hotuba yake kwa kupongeza jitihada zinazochukuliwa na nchi wanachama za kuimarisha mtangamano kama vile uondoaji wa sharti la viza na usuluhishi wa mgogoro wa Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao athari zake inazikumba nchi zote za SADC.
Naye, Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias M. Magosi amewakumbusha washiriki wa Mkutano huo juu ya dira ya maendeleo ya Jumuiya hiyo ambayo imejikita katika maendeleo ya viwanda, kupanua mtangamano wa kikanda, biashara na masoko. Alisema lengo la mkutano huo ni kupitia utekelezaji wa dira hiyo kwa mwaka mmoja uliopita, mafanikio yaliyopatikana na kutafuta suluhu kwa pamoja katika changamoto zilizojitokeza.
Amesema mkutano huo unafanyika wakati dunia inashuhudia changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya siasa za kimataifa, ongezeko la kodi katika biashara na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa misaada kutoka kwa wahisani.
Hayo yote, amesema kuwa yameathiri mtiririko wa biashara na uwekezaji katika kanda, utaratibu uliozoeleka wa kufanya biashara na ugharamiaji wa miradi, changamoto ambazo zinaonekana zinarejesha nyuma jitihada za SADC lakini kwa upande mwingine, amesema zichukuliwe kama fursa kwa nchi wanachama kutafakari namna ya kugharamia
mambo yao wenyewe na kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani ambao mara nyingi misaada yao haina uhakika.
Ameongeza kuwa moja ya malengo ya mkakati wa viwanda wa SADC 2015 -2063 umetoa msisitizo mkubwa wa uendelezaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs), na hasa kutokana na idadi kubwa ya vijana na wanawake kujihusisha na sekta hiyo.
Amebainisha kuwa makundi hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa ujuzi, mitaji, bidhaa/huduma duni na taarifa za masoko. Kuondoa tatizo hilo, Sekretarieti ya SADC imeandaa mkakati wa ushindani kwa sekta ya SMEs unaolenga pamoja na mambo mengine, kuiwezesha sekta hiyo iwe shindani katika Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA).