Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kwa ajili ya kuongoza waombolezaji kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai tarehe 10 Agosti, 2025.
……………
Na Meleka Kulwa – Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Hayati Job Yustino Ndugai, alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda kamati nne za ushauri kwa Serikali kwa ajili ya kuimarisha usimamizi na udhibiti wa rasilimali za nchi, ikiwemo almasi, tanzanite, gesi asilia na mazao ya uvuvi wa bahari kuu.
Akizungumza leo, Agosti 10, 2025, katika Shughuli ya Kitaifa ya kuaga mwili wa Hayati Ndugai iliyofanyika katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Rais Samia amesema kuwa mapendekezo ya kamati hizo yalichangia kuimarisha udhibiti wa rasilimali na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Aidha, amesema kuwa historia itaendelea kumkumbuka Ndugai kama mwanasiasa aliyependa na kuthamini maendeleo ya vijana, kwani alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wanapata elimu. Miongoni mwa walionufaika na jitihada zake ni wasichana, ambapo alijitolea kusimamia upatikanaji wa fedha na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge iliyopo Kikombo, Dodoma.
Akiongoza ibada ya kumuaga Hayati Ndugai, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula, amesema kuwa marehemu alikuwa mtu wa ibada na mwenye kumcha Mungu.
“Mungu Mwenyezi ana uwezo wa kubadili maisha ya familia, mtu binafsi na taifa yakawa mazuri hata kama muda unaonekana umeisha. Usikate tamaa na usichoke kutenda mema, maana hayo ndiyo watu watakayoyakumbuka,” amesema Askofu Gaula.
Kwa upande wake, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, akisoma wasifu wa marehemu, amesema kuwa Ndugai alifariki kutokana na shinikizo la damu kushuka sana (septic shock) lililosababishwa na maambukizi makali ya mfumo wa hewa (severe pneumonia).
Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anna Makinda, amesema, “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Hayati Ndugai kwa sababu nimeishi naye kama mdogo wangu katika kila jambo, na alikuwa mtu mbunifu. Tuishi kwa kujali, maana hatima yetu sote ni hii.”
Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amesema, “Hayati Ndugai alikuwa mwalimu mwema na mtu bora kwangu.” Ameongeza kwa kusema, “Jana mmeona kwa namna wanadodoma walivyojitokeza kwa wingi; hiyo inaonesha kuwa waliokuwa upande wako ni wengi kuliko walio kinyume nawe. Sisi tulio upande wako ni wengi, hivyo Mheshimiwa Rais usiogope.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali kabla ya kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma tarehe 10 Agosti, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma tarehe 10 Agosti, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwafariji wanafamilia wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma tarehe 10 Agosti, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waombolezaji kabla ya kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma tarehe 10 Agosti, 2025.