Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wanachama pamoja na wananchi waliokusanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM (White House) mara baada ya kuchukua Fomu ya kugombea nafasi ya Rais tarehe 09 Agosti, 2025.
………………..
NA JOHN BUKUKU, DODOMA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea wa Nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekabidhiwa rasmi fomu ya ugombea pamoja na Mgombea Mwenza wa CCM, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, katika ofisi za tume hiyo Njedengwa, jijini Dodoma.
Baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Mwenyekiti huyo na Mgombea wa Nafasi ya Urais akizungumza na wana CCM katika Makao Makuu ya chama hicho, maarufu kama White House Dodoma, alisema safari ya kuelekea uchaguzi wa Oktoba imeanza rasmi.
“Safari imeanza, mbio za kuelekea Oktoba sasa zimepulizwa. Kama ni mpira, filimbi imepulizwa na mchezo unaanza. Ifikapo Agosti 28 tutafungua rasmi kampeni zetu, na Oktoba 28 tutazifunga rasmi ili kwenda kuwasikiliza wananchi,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza: “Kama mnavyojua, tumetoka kuchukua fomu na ndio maana tupo hapa. Wahenga walisema: ‘Ukitaka uhondo wa ngoma, ingia ucheze’. Sasa CCM tumeshaingia rasmi na tupo tayari kudemka jinsi ngoma itakavyopigwa. Tupo tayari kucheza na kudemka.”
Dkt. Samia aliwashukuru kwa dhati wanachama wa CCM kwa imani kubwa waliyoonyesha kwake na kwa mgombea mwenza wake. Amesema kuwa serikali inayoongozwa na CCM imefanya mambo makubwa katika sekta zote kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, na hakuna sekta iliyosalia bila kuguswa.
“Mafanikio hayo yapo dhahiri na tumeyafafanua katika hadhara na majukwaa mbalimbali. Niwahakikishie kuwa katika miaka mitano ijayo, tunapoanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, tutafanya mambo makubwa zaidi,” alibainisha.
Amefafanua kuwa safari ya kushindania nafasi ya kufanya mambo haya makubwa inaanza leo, lakini kwa mujibu wa sheria za tume, kampeni zitaanza rasmi Agosti 28. “Tutapita kuwaeleza wananchi na kuomba ridhaa yao. Kwa upande wa CCM, safari imeanza leo mimi na mwenzangu tukiwa tunapeperusha bendera ya chama chetu,” alisema.
Dkt. Samia alisisitiza kuwa hii si safari yake binafsi au ya yeye na mgombea mwenza pekee, bali ni safari ya kila Mtanzania na kila chama cha siasa. Alieleza kuwa ni utaratibu wa kidiplomasia kwa vyama vya siasa kurejea kwa wananchi kila baada ya miaka mitano kutafuta ridhaa ya kuendesha serikali.
“Katika safari hii, wananchi wa Tanzania watachagua chama watakachoona kitawaletea maendeleo na kujenga taifa lenye ustawi, utu, usawa na uchumi imara unaoelekea kujitegemea,” alisema.
Kwa upande wa CCM, alisema yale ambayo chama kinapanga kuyafanya yameelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, yanayolenga kuimarisha uchumi wa viwanda.
Aidha, alibainisha kuwa fomu iliyochukuliwa leo haijakamilika kwa kuwa inahitaji wadhamini kutoka mikoa yote kwa mujibu wa sheria. “Niwaombe wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi na kutoa taarifa sahihi ili tuwe na wadhamini madhubuti,” alisema.
Aliwakumbusha wanachama wote wa CCM kumaliza tofauti baada ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani, na kuungana kwa mshikamano ili kuingia kwenye uchaguzi mkuu wakiwa chama kimoja na madhubuti.
Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa CCM, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, alimshukuru Dkt. Samia na Kamati Kuu ya CCM kwa kumteua na kumthibitisha kuwa mgombea mwenza. “Nipo tayari kushirikiana nawe kikamilifu katika kukipatia ushindi wa kishindo chama chetu,” alisema, akisisitiza kuwa atakuwa msaidizi na si mshindani wake.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Komredi Stephen Wassira, alisema mafanikio ya serikali ya CCM yanaonekana kila kijiji na kwamba hiyo ndiyo silaha yao kuu kuelekea uchaguzi. “Silaha ya pili ni Ilani yetu iliyojaa mambo makubwa. Ikitekelezwa, mwaka 2030 tutakuwa na Tanzania tofauti kabisa na tuliyonayo leo,” alisema, akihitimisha kwa msemo: “La mgambo limelia, safari imeanza.”