
Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Bi. Beatrice Masumbuko akitoa mafunzo kwa Mawakala walioshinda zabuni ya kuuza umeme wa LUKU katika mkoa huo yaliyofanyika katika ukumbi wa TANESCO Training School (TTS), Agosti 7, 2025, Dar es Salaam.

Afisa Habari, Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Temeke Lucia Renatus (wa kwanza kulia) akifatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo mawakala walioshinda zabuni ya kuuza umeme wa LUKU katika mkoa huo.







Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa katika picha ya pamoja na mawakala wapya wa kuuza umeme wa LUKU.
…………..
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limewajengea uwezo mawakala walioshinda zabuni ya kuuza umeme wa LUKU katika mkoa huo, ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wateja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa niaba ya Shirika.
Akizungumza Agosti 7, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa mafunzo kwa mawakala wapya wa kuuza umeme wa LUKU, Afisa TEHAMA Mwandamizi wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Bi. Beatrice Masumbuko, amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha mawakala hao kutoa huduma kwa weledi kwa kuwa wengi wao ni wapya katika utoaji wa huduma hiyo.
Aidha, amewasisitiza mawakala hao kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na TANESCO, sambamba na kuzingatia maadili na uadilifu katika utoaji wa huduma, ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wao, baadhi ya mawakala walioshinda tenda hiyo, akiwemo Bw. Benedict Michael, wamesema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kupata uelewa mpana kuhusu utoaji wa huduma kwa wateja, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika uuzaji wa umeme kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa TANESCO Training School (TTS), ambapo zaidi ya washiriki 40 wamejengewa uwezo ili kufanya kazi kwa ufanisi.