Mratibu wa Michezo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  Bi. Veronica Mtemi akizungumza waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao katika bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) lililofanyika kwenye viwanja vya Masaki Sports Park (MSP) leo Agosti 8, 2025 jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Timu  kutoka NHC, Bw. Said Bungara  akizungumza waandishi wa habari kuhusu  umuhimu wa  bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Wakulima (Nanenane).
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Domina Rwemanyila akitoa elimu kwa washiriki  wa  bonanza la mchezo wa mpira wa miguu kuhusu majukumu mbalimbali ya shirika pamoja na miradi inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa makazi bora nchini.
Nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu  NHC, Bw. Simon Mhiliwa akizungumzia bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Wakulima (Nanenane).
Wachezaji wa Timu ya mpira wa miguuu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiwa uwanjani wakati wakishiriki bonanza.
………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeungana na taasisi mbalimbali nchini kushiriki bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) kwa njia ya michezo ili kutoa nafasi kwa wafanyakazi kupumzika, kuimarisha afya, kukuza urafiki pamoja na kubadilishana uzoefu nje ya mazingira ya kazi.
Akizungumza wakati wa bonanza hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Masaki Sports Park (MSP) leo Agosti 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Michezo kutoka NHC, Bi. Veronica Mtemi, amesema kuwa ushiriki wao katika bonanza hilo umeleta manufaa makubwa kwa umeimarisha ushirikiano baina ya wafanyakazi na taasisi nyingine pamoja na kuboresha afya za washiriki.
“Kwa kutambua umuhimu wa michezo kazini, NHC imeanzisha utaratibu wa kushiriki shughuli mbalimbali za michezo kila siku ya Ijumaa baada ya kazi, ikiwa ni pamoja na riadha,” amesema Bi. Mtemi.
Ameongeza kuwa: “Wafanyakazi wa NHC hushiriki michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, netiboli, karata, bao, pool table ambayo uongeza mshikamano na ari ya kufanya kazi kwa bidii.”
Meneja wa Timu  kutoka NHC, Bw. Said Bungara, amesema kuwa bonanza hilo limekuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya timu yao kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Taasisi za Umma (SHIMUTA), na kuongeza kuwa mashindano hayo yamehusisha timu 10 kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bi. Domina Rwemanyila, ametumia fursa ya kushiriki katika bonanza hilo kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu mbalimbali ya shirika pamoja na miradi inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa makazi bora nchini.
Bi. Rwemanyila amesema kuwa shirika linaendelea kutekeleza miradi ya kisasa ya ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi salama na yenye gharama nafuu.
Amesisitiza kuwa nyumba zinazojengwa na NHC zimezingatia viwango vya juu vya ubora, uimara wa miundombinu, pamoja na mazingira rafiki kwa maisha ya binadamu, huku akieleza kuwa  shirika limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa makazi yanayojengwa si tu yanakidhi mahitaji ya sasa, bali pia yanachangia katika uboreshaji wa mandhari ya miji na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake  Nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu  NHC, Bw. Simon Mhiliwa, amesema bonanza hilo limekuwa chachu ya kuimarisha timu yao na kuongeza morali kwa ajili ya mashindano yajayo. huku akitoa shukrani kwa uongozi wa shirika kwa kuwezesha ushiriki wao na kuonesha dhamira ya kuendeleza michezo kazini.