Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Julian Banzi Raphael, akipata maelezo kutoka kwa Meneja Uendeshaji wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Nkanwa Magina (mwenye kofia) wakati Naibu Gavana alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Wakulima kitaifa katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma tarehe 7 Agosti 2025
………….
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Utawala na Udhibiti wa Ndani), Bw. Julian Banzi Raphael, ameitaka Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuendelea kuuhabarisha umma kuhusu majukumu yake, likiwemo jukumu jipya la kupunguza hasara kwa benki.
Ameyasema hayo tarehe 7 Agosti 2025 wakati alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Naibu Gavana ameitaka DIB kuwa mwangalifu katika utekelezaji wa jukumu hilo jipya la kupunguza hasara, ili benki zisije zikatumia fursa hiyo ya kukwamuliwa na DIB vibaya.
“Ni vizuri muwe waangalifu katika kutekeleza jukumu la kupunguza hasara kwa benki kwa kuhakikisha jukumu hilo halitumiwi vibaya na benki ili muweze kufikia matarajio yenu ya kurejesha benki katika uimara wake, badala ya kila mara kutumia fedha nyingi kulipa fidia wakati benki zinapofilisika,” alisema Naibu Gavana Raphael.
Katika banda hilo, Meneja Uendeshaji wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Nkanwa Magina, alimweleza Naibu Gavana kwamba kuna mwitikio mzuri wa wananchi kujifunza kuhusu DIB na kwamba wanatumia maonesho haya pia kuwaeleza kuhusu jukumu jipya la kupunguza hasara kwa benki, na kwamba wengi wameonesha kufurahishwa na kazi inayofanywa na DIB.
“Jukumu hili la loss minimizer (kupunguza hasara) limepokelewa vizuri kwa kuwa linatufanya DIB kuchukua hatua mapema kuzisaidia benki na taasisi za fedha zilizo katika mgogoro ili kuzikwamua ziendelee na biashara, badala ya kusubiri hadi zinapokufa na kulipa fidia ambayo inaweza kuwa ya gharama kubwa zaidi,” alisema.
Bw. Magina amesema zoezi linaloendelea sasa ni kuandaa kanuni za kusimamia utekelezaji wa jukumu hilo, ambalo linatarajiwa kuwa litakuwa la nafuu zaidi kwa shirika kuliko kama taasisi zingeachwa hadi zife au zifilisike na yafanyike malipo ya fidia.
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ni taasisi ambayo kwa muda mrefu imekuwa sehemu ya Benki Kuu ya Tanzania na kwamba ni hivi karibuni imeanza kujitegemea katika baadhi ya majukumu. Hata hivyo, utendaji wa DIB unahusiana sana na Benki Kuu ambayo ina jukumu la kusimamia na kukagua benkji na taasisi za fedha. Hata utekelezaji wa jukumu jipya la DIB la kupunguza hasara kwa benki, utategemea usimamizi wa benki unaofanywa na Benki Kuu.
Katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka huu, DIB pia inashiriki huko Zanzibar na katika kanda za Kaskazini jijini Arusha, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya na Kanda ya Mashariki jijini Morogoro.