Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Kanyeka (kushoto)akitoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye banda la shirika hilo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo Jijini Mwanza.
Afisa Udhibiti Ubora Bi.Shija Jackson akitembelea wajasiriamali katika maonesho ya Nanenane Yanayofanyika Nyamhongoro wilayani Ilemala mkoani Mwanza.
Baadhi ya wananchi wakipata elimu kwenye banda la TBS.
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeeleza kuwa maonesho ya wakulima Nane Nane mwaka 2025 yamekuwa fursa muhimu kwao kukutana na wadau mbalimbali kutoka sekta mbalimbali ikiwemo sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hivyo kupata fursa ya kutoa elimu kuhusu masuala ya viwango pamoja na udhibiti ubora.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 6, 2025 katika viwanja vya Nyamh’ongolo mkoani Mwanza, Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Kanyeka alisema bidhaa nyingi zinazotokana na sekta hizo ndizo zinazothibitishwa na kukaguliwa na shirika hilo.
“Tuna viwango vya bidhaa za mazao kama unga, mchele, hizo ni bidhaa za kilimo, nyama, maziwa, soseji ni bidhaa za mifugo na samaki ni bidhaa za ufugaji. Kupitia maonesho haya, tumekutana na wadau hao tumewapa elimu kuhusu umuhimu wa alama ya ubora na namna ya kuzipata,” alisema Kanyeka.
Aidha, alisema kuwa mbali na wananchi kutembelea banda la TBS na kupata elimu, shirika hilo pia limetembelea na kukutana na wajasiriamali mbalimbali waliopo katika maonesho hayo na kuwashauri umuhimu wa kupata alama ya ubora ikiwemo na kuwasikiliza changamoto zao.
“Tumeona bidhaa zilizo na alama ya ubora ambazo zimekidhi matakwa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara, Lakini kwa bidhaa ambazo hazina alama ya ubora, tumetoa elimu ya taratibu zinazopaswa kufuatwa ili ziweze kupata alama hiyo,” alieleza Kanyeka.
Kanyeka alibainisha kuwa TBS inatoa huduma ya alama ya ubora bure kwa wajasiriamali wadogo wanaotambuliwa na SIDO, na kuwahimiza kuwasiliana na TBS kwa ajili ya huduma zaidi.
“Tunataka wafahamu kuwa TBS si chombo cha kukamata bali ni taasisi inayosaidia wajasiriamali kukua. Tunapokuta bidhaa haijafikia viwango, tunatoa ushauri na tunawezesha pia alisema.
Skampam Elirehema, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TBS, alisema amejifunza mambo mengi kuhusu namna ya kutambua bidhaa zenye ubora kupitia alama ya TBS na umuhimu wa kusoma maelezo kwenye vifungashio vya bidhaa.
“Nimegundua kuwa kuna bidhaa zingine tunazitumia tofauti na maelekezo yaliyopo kwenye kifungashio.Elimu hii imenisaidia sana,” alisema.
Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi kama TBS kutoa elimu, kusikiliza changamoto za wadau na kusaidia kuboresha bidhaa na huduma katika soko la Tanzania.