Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Agosti 5,2025
Katika zoezi la kupiga kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Bagamoyo , kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),aliyekuwa Mbunge viti maalum mkoani Pwani, CPA Subira Mgalu ameongoza kwa kupata kura 3,544.
Katika matokeo yaliyotangazwa rasmi na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Shaban Karage alisema wagombea walikuwa watano wakichuana kuwania tiketi ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Karage alifafanua kuwa, jimbo hilo lina kata 11 , kura zilizopigwa 5,567, zilizoharibika 232 ambapo kura halali zilikuwa 5,535.
Mgalu anaongoza akifuatiwa na Mbunge aliyemaliza muda wake jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge aliyepata kura 1,574 , wengine ni Christina Henry kura 133, Hajji Ngwila kura 47, na Matasi Kambi kapata kura 37.
Mchakato huu umefuata taratibu za ndani ya chama, na matokeo haya yatawasilishwa kwa ngazi ya mkoa kisha ngazi za juu kwa hatua na taratibu zaidi za kichama.